• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:10 PM
Suarez kujiunga na Atletico Madrid

Suarez kujiunga na Atletico Madrid

Na MASHIRIKA

BARCELONA wamekubali kumwachilia mshambuliaji Luis Suarez ajiunge na washindani wakuu katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Atletico Madrid.

Suarez hatakikani kabisa kambini mwa Barcelona ambao kwa sasa wanatiwa makali na kocha mpya Ronald Koeman. Miamba hao wa soka ya Uhispania walikuwa radhi kumwachilia Suarez ambaye ni raia wa Uruguay kujiunga na kikosi chochote bila ada ilmradi klabu ambayo angejiunga nayo si ya La Liga.

Suarez alihiari kupunguziwa mshahara ili kuingia katika sajili rasmi ya Atletico baada ya uhamisho wake hadi Juventus ya Italia kugongwa mwamba kwa sababu ya changamoto za kutafuta pasipoti na kibali cha kufanyia kazi Italia.

Rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu alizuia uhamisho wa Suarez hadi Atletico kwa sababu hakutaka nyota huyo auzwe kwa kikosi ambacho ni washindani wao wakuu ligini.

Hata hivyo, baada ya kukutana na wawakilishi wa Suarez, vinara wa Barcelona waliafikiana nao baada ya fowadi huyo wa zamani wa Liverpool kufichua mipango ya kuanika kwenye vyombo vya habari jinsi “anavyohangaishwa” na Barcelona.

Atletico kwa sasa wameweka mezani kima cha Sh448 milioni kwa minajili ya huduma za Suarez mwenye umri wa miaka 33.

Hata hivyo, fedha hizo huenda zikaongezeka kutegemea jinsi Suarez atakavyowajibishwa na Atletico na iwapo ataongoza kikosi hicho cha kocha Diego Simeone kupiga hatua zaidi kwenye soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Uhamisho wa Suarez unatamatisha kipindi cha miaka sita ya usogora wake kambini mwa Barcelona ambao amewafungia jumla ya mabao 198 kutokana na mechi 283. Katika enzi za ubora wake, Suarez alishirikiana vilivyo na Lionel Messi na Neymar muungano wao almaarufu MSN ukawa tishio zaidi kwa mabeki wa kikosi chochote duniani.

Suarez alijiunga na Barcelona mnamo 2014 baada ya kuagana na Liverpool kwa kima cha Sh10.3 bilioni. Tangu wakati huo, ameshindia Barcelona mataji manne ya La Liga, manne ya Copa del Rey, moja la UEFA na jingine la Kombe la Dunia mnamo 2015.

You can share this post!

Alvaro Morata arudi Juventus kwa mkopo kutoka Atletico...

Beki Ruth Ingosi wa Harambee Starlets ajiunga na AEL...