• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 2:56 PM
Fuo za bahari kufunguliwa wiki ijayo

Fuo za bahari kufunguliwa wiki ijayo

Na MISHI GONGO

MIKAKATI ya kufungua fuo za Bahari Hindi zilikuwa zimefungwa katika Kaunti ya Mombasa kwa muda wa miezi saba kutokana na janga la corona, imeanza.

Akizungumza na wanahabari, kamishna wa Mombasa Bw Gilbert Kitiyo amesema wameweka taratibu ambazo zitatekelezwa na watu watakaozuru eneo hilo.

“Tunafanya majadiliano kuona kuwa fuo za bahari zinafunguliwa wiki ijayo, lakini kabla ya hapo tunajali mikakati itakayofuatwa,” amesema.

Amesema miongoni mwa masharti hayo ni watu kunawa na kuvalia maski wanapozuru eneo hilo.

Amesema hayo Jumatano akihutubia wanahabari katika kongamano la idara za usalama.

Amesema wamefikia hatua hiyo baada ya Rais Uhuru Kenyatta siku ya Jumatatu kuagiza kufunguliwa kwa bustani ya Mama Ngina.

“Tumefanya hivyo ili kuwapa wakazi sehemu zaidi za kujiburudisha. Hata hivyo tunawasisitiza wasilegeze masharti yaliyowekwa na wizara ya afya,” akasema.

Aidha amewaonya wakazi ambao hawatekelezi masharti hayo akisema watachukuliwa hatua.

Wakati huo huo amewaonya wakazi ambao wanakiuka kafyu.

“Tumetambua kuwa kuna baadhi ya watu ambao wanakiuka kafyu ambapo wanatoka nje usiku na wanaponaswa na maafisa wa usalama hujaribu kuwahonga,” akasema.

Sehemu zingine zilizofungwa ni mikahawa, hoteli, pamoja vilabu vya densi na vile vya pombe.

Wakiagiza kufungwa kwa sehemu hizo mwezi Machi gavana wa Mombasa Bw Hassan Joho na Kamishna wa Kaunti hiyo Bw Gilbert Kitiyo walisema kuwa Mombasa iko katika hatari zaidi ya kuandikisha idadi kubwa ya ugonjwa huo kutokana na kuwa na viingilio ambavyo ni uwanja wa ndege wa Moi na Bandari; hivyo wageni kutoka mataifa mbali mbali hutumia kuingilia nchini.

Kufungwa kwake kuliwaathiri wauzaji chakula katika eneo hilo pakubwa.

  • Tags

You can share this post!

ANA KWA ANA: Amebobea kufuma sweta, kofia akitumia sindano...

Semedo ajiengua Barcelona na kutua Wolves kwa Sh5.2 bilioni