DCI yataka Malala ashtakiwe

Na MARY WANGARI

MKURUGENZI wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), George Kinoti anataka Seneta wa Kakamega Cleophas Malala ashtakiwe kwa kutoa ‘madai ya uongo’ kuhusu njama ya kumuua.

Mnamo Septemba 14, 2020, Bw Malala alibubujikwa na machozi hadharani katika kikao cha kamati ya Seneti akisema kwamba maisha yake yamo hatarini.

Akihojiwa Jumatano mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Haki, Masuala ya Sheria na Haki za Binadamu, Bw Kinoti alisema hakukuwa na ushahidi wowote wa kuthibitisha madai ya Seneta Malala.

“Kulingana na ushahidi uliorekodiwa, tumepata madai ya Malala kuwa ya uongo, kisasi na yenye nia mbaya. Aliyetoa madai hayo anapaswa kushtakiwa kwa kutoa habari za uongo,” alisema Bw Kinoti.

Alieleza kuwa Bw Malala alikataa kutoa habari muhimu kuhusu maafisa wa Kikosi cha Huduma Maalum (SSU) aliodai walikuwa wametwikwa jukumu la kumwandama na kumwangamiza.

“Hata nilimwambia ikiwa ni maafisa wetu basi atoe picha lakini akakataa,” akasema.

“Maafisa wa uchunguzi walimwagiza Malala kuwapa tarehe halisi alipoandamwa na nambari za simu na picha za maafisa aliodai wameamrishwa kumuua,” alisema.

DCI sasa inamtaka Bw Malala kuomba msamaha Kikosi cha Huduma Maalum (SSU) akisema kwamba madai ya Seneta huyo yameathiri sifa za maafisa wa kikosi hicho.

“Madai hayo yanayogusa sifa za maafisa wa SSU yamefanya maafisa hao kukumbana na dhihaka na kudhalilishwa machoni pa umma,” alihoji.

Huku akitaka kuongezewa ulinzi, seneta huyo alikuwa amedai kuwa kundi la maafisa watano kutoka SSU waliojihami kwa silaha kali walikuwa wameagizwa kumwandama na kumwangamiza.

Wakati huo huo, Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai aliwahakikishia viongozi ambao walikuwa wamepokonywa walinzi kwamba watarejeshewa.

Alisema kuwa afisi yake imejitolea kuhakikisha uhuru wa Idara ya Polisi.