• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 10:06 AM
TAHARIRI: Wadau wasisahau masuala muhimu

TAHARIRI: Wadau wasisahau masuala muhimu

Na MHARIRI

JUMATATU ijayo wadau wanakutana kujadili jinsi Kenya itakavyosonga mbele baada ya janga la Covid-19, ambalo limetukumba kwa nusu mwaka.

Siku hiyo, walimu watakuwa wakirejea shuleni kujiandaa na ufunguzi, ambao kuna uwezekano ukawa mwanzoni mwa Oktoba.

Sekta ya elimu ni kati ya zilizoathiriwa vibaya na corona. Hakuna uhakika kama shule nyingi za kibinafsi zitafunguliwa. Hata zikifunguliwa, baadhi ya walimu watakuwa na shughuli nyingine za kuwapatia riziki. Walimu wengi katika shule hizo ambazo hutegemea karo ya wanafunzi, wamekuwa bila mshahara kwa miezi hiyo sita.

Kadhalika kuna walimu walioajiriwa na bodi zinazosimamia shule. Serikali ilitangaza kwamba ilitoa pesa za kuwalipa. Wengi wanalia kuwa hawajapokea malipo hayo.

Suala kubwa linalofaa kuangaziwa kabla ya kuzifungua shule ni kuhusu miundomsingi muhimu.

Waziri wa Elimu Prof George Magoha ameendelea kufuatilia uundaji wa madawati. Mpango huo unalenga kupunguza msongamano katika shule, kama mojawapo ya njia za kuwakinga wanafunzi na maambukizi ya corona.

Kununua madawati bila ya kujua wanafunzi watasomea wapi, ni kutofikiria kwa hekima. Shule nyingi za umma hazina vyoo vya kutosha, maji safi, madarasa na walimu wa kutosha.

Prof Magoha hajaeleza kama kutaongezwa madawati na darasa tayari limejaa, madawati hayo yatawekwa wapi. Na iwapo yatapelekwa nje ya madarasa, labda chini ya mahema, ni kigezo gani kitakachotumiwa kuwaacha baadhi ya wanafunzi ndani na kuwapeleka wengine wakae nje?

Tangu kuanzishwa kwa mpango wa Elimu bila Malipo katika shule za msingi (FPE), kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi huku walimu wakiwa wachache.

Tume ya Huduma za Walimu (TSC) imetangaza nafasi za kazi lakini haijaeleza kama walimu hao watajaza pengo litakalotokea, iwapo wanafunzi katika shule za kibinafsi watajiunga na za umma.

Prof Magoha wiki hii alinukuliwa akijibu kimzaha kwamba wanafunzi katika shule za wamiliki binafsi wanakaribishwa katika shule za umma.

Kenya ina zaidi ya shule za wamiliki binafsi 8,000 na maelfu ya wanafunzi.

Wadau watakapojadili mustakbali wa nchi, wasisahau kuangazia uwezekano wa watoto hao kukosa nafasi ya kusoma.

You can share this post!

‘Nchi nyingi hazithamini usalama wa wahamiaji na watafuta...

NGILA: Ushirikiano kiteknolojia utapunguza maambukizi