Habari Mseto

Wacheza densi wa kigeni waliokolewa na polisi, korti yaambiwa

September 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

WASAKATAJI densi wa kunengua viuno tisa waliokuwa wameingizwa nchini kutoka mataifa ya Nepal na Pakistan kinyume cha sheria waliokolewa na maafisa wa polisi kutoka kilabu kimoja Nairobi walipokuwa wanatumiwa vibaya, hakimu mkuu wa Nairobi Bw Francis Andayi amefahamishwa.

Bw Andayi alielezwa na afisa wa polisi kutoka kituo maalum cha kupambana na uhalifu wa kimataifa (Tuoc) Koplo Judith Kimungui kwamba polisi waliingia katika kilabu kijulikanacho kwa jina Balle Balle kilichoko Parklands Nairobi kuwaokoa wasichana hao.

Wasichana hao kutoka nchi za Nepal na Pakistan walikutwa wakinengua matako na kuzungusha viuno huku wanaume 14 wa asili ya Kiheshia na wanaume Waafrika 11 walikuwa wanawakondolea macho huku wakiendelea na kubugia vinywaji.

Polisi walikuta ndoo 10 zilizokuwa zimewekewa kila msichana za kuwekwa pesa na wateja ndani ya kilabu hicho.

Kutoka afisi ta mmiliki wa kilabu hicho polisi walichukua Sh315,000 za Dola za Marekani 129 (Sh12,900).

Polisi walikuta wasichana hao walikuwa wamenyang’anywa pasipoti zikafichwa na wenye kilabu hicho.

Wasichana hao walikuwa wameishi nchini kenya kati ya Feburuari na Julai 2019.

Koplo Kimungui aliyekuwa akitoa ushahidi dhidi ya wenye kilabu hicho cha Balle Balle Mabw Shaikh Furoan Hussain na Abduk Waheed Khan alisema wasichana hao walitoroka kwa kasi ya umeme polisi walipoingia kilabuni.

“Wasichana hao waliokuwa wameingizwa nchini na Hussain walitoroka kwa kasi ya umeme kutoka jukwaani walipokuwa wanasakata densi kwa kunengua viuno na kutia machachari ya miondoko kutoka mashariki ya mbali,” hakimu alielezwa.

Mle jukwaani , Koplo Kimungui alisema kulikuwa kumekwa ndoo 10 ambazo ziliwekwa pesa na watazamani wa densi hiyo kutoka Nepal na Pakistan.

Afisa huyo wa uchunguzi wa jinai unaojumuisha mataifa ya kigeni, alisema walipashwa habari za maalum kwamba “ wasichana wa umri mdogo walikuwa wananyanyaswa katika kilabu kimoja jijini Nairobi.”

“Kundi kubwa la maafisa kutoka vitengo mbali mbali vya serikali vya kutetea haki za watoto na wanawake zilifika katika Club cha Balle Balle Parklands usiku wa Julai 18,20919 kutekeleza oparesheni ya kuwaokoa watoto hao,” Koplo Kimungui alisema akitoa ushahidi dhidi ya Hussain na Khan.

Hussain na Khan wanakabiliwa na mashtaka matano ya ukiukaji wa haki za binadamu kuwaajiri wasichana hao tisa kucheza densi katika kilabu cha Balle Balle na pia kufanikisha usafiri wa wasichana hao kutoka Nepal na Pakistan hadi Nairobi.

Wawili hao wameshtakiwa kukaidi haki za wasichana hao kwa kuficha pasipoti zao na kuwafungia katika jumba moja jijini Nairobi.

Hakimu alielezwa baada ya polisi na maafisa wengine kutoka idara ya kutetea haki za watoto waliwafuata unyounyo wasichana hao waliokuwa wamejificha katika chumba kimoja kilabuni humo.

Hakimu alijuzwa wasichana hao waliokolewa na kupelekwa katika jumba moja ambapo walifungiwa ndipo umri wao upimwe ibainike ikiwa walikuwa watoto ama watu wazima.

Ilibainika wasichana hao walikuwa na umri wa miaka zaidi ya 18.

Hatimaye wasichana hao walisafirishwa na Serikali na kurudishwa nchini Nepal na Pakistan na idara ya uhamiaji.

Mabw Hussain na Khan wamekanusha mashtaka dhidi yao na wako nje kwa dhamana.

Kesi iliahirishwa hadi Oktoba 1 na 5, 2020.