• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Jinsi kilimo kilivyomwokoa mwalimu kutoka kwa meno ya ngwena Covid-19

Jinsi kilimo kilivyomwokoa mwalimu kutoka kwa meno ya ngwena Covid-19

Na BENSON MATHEKA

LICHA ya shule kufungwa kutokana na janga la Covid-19, mwalimu mmoja wa chekechea alikata kauli kujituma kikamilifu katika kilimo na amefua dafu.

Jonah Mwanzia ametambua kuwa akili ni mali na ameondokea kuwa mkulima maarufu wa French beans maarufu kwa jina mishiri.

Mwanzia, aliye mwalimu wa shule ya chekechea ya Kitoi alizaliwa katika kijiji cha Kiteng’ei, kata ya Iveti, Kaunti ya Machakos yapata miaka 32 iliyopita. Aliamua kujitosa mzimamzima katika bahari pana ya kilimo baada ya janga la corona kukatiza mahali ambako alikuwa akitegemea kujitafutia mkate wa kila siku.

“Nilipong’amua kuwa shule zimefungwa kote nchini kutokana na kuenea kwa virusi vya corona, niliona ni heri niingilie zaraa, angalau nizidi kusukuma gurudumu la maisha’’ asema mkulima huyu.

Mwanzia asema kwamba, alitumia kiasi kidogo cha pesa alizokuwa akihifadhi kama mtaji kuanza kilimo.

Aliongezewa pia Sh2,000 na rafikiye mmoja ili kumpiga jeki katika zaraa hii. Babake pia alimgawia shamba la ekari mbili ili aendeleze kilimo.

“Babangu alinigawia kijisehemu cha shamba, karibu na chemichemi ya maji ili niendeleze ukulima wangu,’’ asema.

Mkulima huyu adokeza kwamba, tangu alipoanza kazi hii, amepata tija na kufua dafu kimapato, na hata akawapiku wenzake wanaochapa kazi maofisini.

”Nimefana mno kimaisha kupitia kazi ya mikono yangu. Corona imeleta baraka kwangu maana nimetambua kuwa kilimo ndicho uti wa mgongo katika ufanisi wa jamii.Napata hela nyingi kuliko zile nilizokuwa nalipwa na wazazi shuleni,” asema mkulima huyu.

Mwanzia asema ‘mishiri’ huchukua kati ya siku 45 na 60 kukomaa baada ya kupandwa, bora mkulima afuate kikamilifu ushauri kutoka kwa maafisa wa kilimo walio nyanjani.

Jonah Mwanzia. Picha/ Benson Matheka

Anaarifu kwamba,katika shamba lake, huwa anavuna zaidi ya kilo 8,000 kwa msimu.

“Hata hivyo,,hii hutegemea jinsi ambavyo nimeitunza mimea hiyo kwa kutia rotuba, kunyunyiza maji mara mbili kwa siku na pia kunyunyiza dawa za kuua wadudu,” aeleza.

Mkulima huyu huwa anauza mazao yake moja kwa moja kwa kampuni ya Fresh Beans iliyoko mjini Thika bila kutegemea mawakala. Hii imemfanya afurahie matunda ya jasho lake maana malipo ni ya kuridhisha.

Anasema ni rahisi kuanza kulima mishiri kwa sababu, mbegu hupandwa moja kwa moja shambani. Baada ya muda wa wiki moja, mmea huo huota na kuchipuza.

“Mmea huo ukiota matawi, mkulima ni lazima anyunyizie dawa ya kuua wadudu waharibifu na kuhakikisha ya kwamba shamba lake lina rotuba itakikanavyo,’’ ashauri .

Anazidi kusema kwamba, ukuzaji wa ‘mishiri’ hauna gharama kubwa kama watu wengi wanavyodhania; bora mkulima awe amejiandaa vilivyo kukabiliana na changamoto zozote zile.

Hata hivyo, hakuna masika yasiyo na mbu. Mkulima huyu asema kwamba, ukosefu wa soko bora nyakati nyingine huwapatia wakulima hasara kubwa na pia kuna suala nyeti la mawakala wanaonunua mavuno yao kwa bei duni kabisa huku wakipata faida nono kupitia jasho lao.

‘’Ingawa mimi sitegemei mawakala kununua mazao yangu, kwa niaba ya wenzangu, naomba serikali ya kaunti ya Machakos idhibiti ununuzi wa ‘mishiri’ ili tupate kulindwa kutoka kwa minyororo ya mawakala walafi,’’ asema.

Ili kudhihirisha ya kwamba kilimo hulipa, mkulima huyu ameajiri wafanyi kazi wanne wanaomsaidia katika kutunza , kuvuna mazao hayo huku yeye mwenyewe  akiwa pia meneja mkuu anayehusika na masuala ya soko na kuweka rekodi za mauzo.

‘’Sitaacha kilimo hata Covid-19 ikidhibitiwa na shule kufunguliwa. Nitazidi kutia bidii ya mchwa katika zaraa hii ili niwe mkwasi wa kutajika janibu za Ukambani na kuwa mfano wa kuigwa katika jamii huku pia nikiendelea na kazi yangu ya ualimu,’’ asema.

Mkulima huyu anawashauri vijana waingilie kazi ya ukulima badala ya kuingilia hulka zinazoweza kusambaratisha ndoto zao za kufana siku za usoni.

“Vijana wajue kuwa ajizi ni nyumba ya njaa na wajitume kikamilifu katika fani ya kilimo na kamwe hawatajuta maishani mwao’’ asema mkulima huyu.

You can share this post!

Leeds United wasajili Llorente kutoka Real Sociedad

Kocha Bilic wa West Brom apigwa faini ya Sh1.1 bilioni kwa...