Ugonjwa 'ajabu' waua mbwa 20 Munyu
Na LAWRENCE ONGARO
WAKAZI wa kijiji cha Munyu, Thika Mashariki, wana hofu kutokana na ugonjwa wa ajabu unaoangamiza mbwa wao.
Walisema ya kwamba kwa muda wa miezi miwili iliyopita wamepoteza mbwa 20 ambao wamefariki kiholela bila kuelewa kiini chake.
Wakazi hao walidai ya kwamba mbwa hao huonekana kudhoofika na zikishapita siku chache, wanaanza kutoa manatoa kamasi kutoka puani huku wakikohoa bila kusita na kwa muda mchache hufa.
“Jambo hilo limetuacha na maswali mengi tusijue la kufanya. Tumejaribu kufanya uchunguzi kuelewa kitandawili hicho bila mafanikio,” alisema Peter Waweru ambaye ni mkazi ya kijiji hicho cha Munyu.
Mwingine naye akasema amepata hasara.
“Mimi pia nimepoteza mbwa wangu ambaye alikuwa kama mlinzi wangu wa boma. Sisi kama wakazi wa eneo hili tumebaki na maswali mengi bila majibu,” alisema Bw Waweru.
Maafisa wa afya ya mifugo walifika mahali hapo ambapo wanaendelea kufanya uchunguzi wao ili kubainisha chanzo cha mbwa kufa.
Jambo hilo limewaacha wakazi hao na wasiwasi tele huku wakihofia maisha yao pia.
“Tungetaka serikali kuingilia kati na kuhakikisha maisha ya binadamu na wanyama yanalindwa vilivyo ili kusiwe na janga hatari la maradhi yanayoweza kuzuka ghafla,” alisema James Kamau ambaye ni mkazi wa kijiji hicho.