• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 10:55 AM
Agizo polisi warudishe sare za zamani

Agizo polisi warudishe sare za zamani

Na MARY WAMBUI

WAKUU wote wa polisi katika Kaunti ya Nairobi wamepewa hadi leo Ijumaa jioni kuwasilisha sare zao za zamani kwa hifadhi ya Idara ya Polisi nchini Kenya katika eneo la Industrial Area, Nairobi.

Hilo linafuatia agizo lililotolewa na Kamanda Mkuu wa Polisi wa Nairobi, Bw Rashid Yakub mnamo Jumatano. Wakuu waliopewa agizo hilo ni wale wanaosimamia vituo vya kaunti-ndogo, trafiki, mabohari, mahakama kati ya idara nyingine.

“Tafadhali hakikisha kwamba umewasilisha cheti maalum kuonyesha kuwa sare hizo zimewasilishwa na haziko tena mikononi mwa polisi husika. Shughuli hii inapaswa kukamilika kufikia Ijumaa,” likaeleza agizo hilo.

Duru ziliiambia Taifa Leo kuwa sare hizo zitatupwa ama kuwekwa mahali palipofichwa ili kuzuia hali ambapo zinaweza kuanza kuuzwa jijini.

Agizo hilo pia linamaanisha kuwa huenda mafundi wa nguo ambao wamekuwa wakiwauzia baadhi ya polisi sare hizo kinyume cha sheria wakaendelea kupata faida.

Kuna hofu kuwa huenda wahalifu wakatumia sare hizo mpya kuendeleza uhalifu kwa kuwahangaisha raia.

Duru zilisema baadhi ya mafundi wamekuwa wakihadaiwa na watu ambao si polisi kuwashonea sare hizo, kwani wengi huwa hawafanyi juhudi kuchunguza ikiwa watu hao ni polisi au la.

“Maswali pekee ambayo wamekuwa wakiuliza ni kituo anakohudumu mtu na kiwango anachoshikilia.

“Nilimpigia simu fundi mmoja ambapo nilimwahidi nitaenda kwake ili kuchukua vipimo vyangu. Hata hivyo, sikuenda kwani sikuwa nahitaji sare. Alianza kunipigia simu akinirai kuiendea haraka kwa ahadi kuwa atanipunguzia malipo,” akasema polisi ambaye hakutaka kutajwa.

Kwa mujibu wa sheria za polisi, ni makosa kwa mtu yeyote kupatikana na sare za polisi bila kibali.

“Mtu yeyote ambaye si polisi atakayepatikana na sare ya polisi bila kuelezea sababu za kutosha alivyoipata atashtakiwa,” inaeleza sheria.

Sheria pia inasema polisi yeyote anayeuza ama kupoteza sare yake bila kutoa sababu za kutosha huenda akafungwa miezi sita gerezani ama kupigwa faini isiyozidi Sh500,000 ama kupewa adhabu zote mbili.

  • Tags

You can share this post!

Eldonets wachomoa wanavikapu matata kutoka vyuoni

Pensheni: Bunge lakataa ushauri wake Uhuru