• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 2:10 PM
Pensheni: Bunge lakataa ushauri wake Uhuru

Pensheni: Bunge lakataa ushauri wake Uhuru

Na CHARLES WASONGA

MAKABILIANO makali yanatarajiwa kati ya wabunge na Rais Uhuru Kenyatta kuhusu mswada unaopendekeza pensheni ya Sh100,000 kila mwezi kwa wabunge waliohudumu kati ya 1984 na 2001.

Kamati ya Bunge kuhusu Fedha imetupilia mbali memoranda ya Rais Kenyatta iliyopinga malipo hayo, na ikawataka wabunge wote 349 kukubaliana na uamuzi huo.

“Baada ya kamati hii kuchanganua pingamizi za Rais kuhusu Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Pensheni ya Wabunge, 2019, inapendekeza kuwa bunge likubaliane na uamuzi wake wa kupinga memoranda ya Rais,” kamati hiyo ikasema kwenye ripoti yake iliyowasilishwa bungeni Alhamisi na mwenyekiti wake, Bi Gladys Wanga.

Kamati hiyo ilisema kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha, wabunge wa zamani wanaishi maisha ya uchochole kwani pesa ndogo wanazopata haziwezi kukimu mahitaji yao.

“Rais alikosa kuzingatia kuwa wabunge hawa wa zamani wanapitia changomoto nyingi maishani, baada ya kutumikia taifa hili kwa uadilifu, kwa sababu hawawezi kupata ajira kwingine,” wabunge wanachama wa kamati hiyo wakasema katika ripoti yao.

Sasa uamuzi wa kamati hii sharti upate uungwaji mkono na angalau thuluthi mbili ya wabunge wote, (sawa na wabunge 233), kulingana na kipengee cha 115 cha Katiba.

Hapo ndipo mswada huo utakapoweza kuwa sheria kinyume na matakwa ya Rais, jambo ambalo halijawahi kutendeka katika historia ya taifa hili.

Mnamo Septemba 10, 2020 Rais Kenyatta alidinda kutia saini mswada huo na kuurejesha bungeni na maelezo ya kuwataka wabunge waondoe kipengele cha 2 kinachopendekeza kuwa karibu wabunge 290 wawe wakitia kibindoni Sh100,000 kila mwezi.

 

  • Tags

You can share this post!

Agizo polisi warudishe sare za zamani

Korti yaelezwa jinsi wanenguaji viuno raia wa kigeni...