Habari Mseto

Korti yaelezwa jinsi wanenguaji viuno raia wa kigeni walivyookolewa na polisi

September 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

WASAKATAJI densi tisa waliokuwa wameingizwa nchini kutoka mataifa ya Nepal na Pakistan kinyume cha sheria, waliokolewa na polisi kutoka kilabu kimoja Nairobi walipokuwa wanatumiwa vibaya, hakimu mkuu wa Nairobi, Bw Francis Andayi alifahamishwa Alhamisi.

Bw Andayi alielezwa na afisa wa polisi kutoka kituo maalum cha kupambana na uhalifu wa kimataifa (Tuoc), Koplo Judith Kimungui kwamba polisi waliingia katika kilabu kijulikanacho kwa jina Balle Balle kilichoko Parklands, Nairobi kuwaokoa wasichana hao.

Wasichana hao kutoka Nepal na Pakistan walikutwa wakinengua viuno huku wanaume 14 wa asili ya Ashia na wengine 11 wa Kiafrika wakiwakodolea macho huku wakiendelea na kubugia vinywaji.

Polisi walikuta ndoo 10 zilizokuwa zimewekewa kila msichana za kutiwa pesa na wateja ndani ya kilabu hicho. Polisi walichukua Sh315,000 za Dola za Marekani 129 (Sh12,900). katika kilabu hicho. Wasichana hao walikuwa wamenyang’anywa paspoti zilizofichwa na wenye kilabu hicho.