• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Wabunge wakataa mswada unaolenga kuwapa madiwani nafasi kusimamia maendeleo

Wabunge wakataa mswada unaolenga kuwapa madiwani nafasi kusimamia maendeleo

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wamezima ndoto ya madiwani ya kusimamia hazina za kufadhiliwa miradi ya maendeleo katika wadi zao.

Mnamo Alhamisi wabunge walikataa kuidhinisha Mswada wa Hazina ya Maendeleo katika Wadi, 2018 ambao ulidhaminiwa na kiranja wa wengi Irungu Kang’ata.

Hazina hiyo ilitarajiwa kufanya kazi sawa na Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge (NG-CDF) ambayo hutengewa fedha na Hazina ya Kitaifa na kusimamiwa na wabunge.

Mswada huo wa Bw Kang’ata ambaye pia ni Seneta wa Murang’a, ulikuwa unapendekeza kila mojawapo ya wadi 1,445 nchini itengewe angalau asilimia 15 ya jumla ya fedha za maendeleo kwa wadi.

Mswada huo ulipata uungwaji mkono mkubwa katika Seneti mwaka 2019 na ukawasilishwa kwa Bunge la Kitaifa. Lakini mnamo Alhamisi wabunge waliukataa.

Sasa mswada huo utawasilishwa kwa Kamati ya Upatanisho utakaojumuisha idadi sawa ya wanachama kutoka bunge la kitaifa na Seneti.

Majina ya wanachama wa kamati hiyo yatapendekezwa, kwa pamoja na Maspika Justin Muturi (Bunge la Kitaifa) na Kenneth Lusaka (Seneti).

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bw Kang’ata alisema alivunjwa moyo na kukataliwa kwa mswada huo katika bunge la kitaifa lakini akaelezea matumaini kuwa muafaka utapatikana kuuhusu katika Kamati ya Upatanisho.

“Bado kuna nafasi. Mswada huu unaweza kunusuriwa,” akasema.

Hata hivyo, Bw Kang’ata aliwataka madiwani kote nchini kuwashawishi wabunge wakubaliane na mswada ambao alisema utachochea maendeleo katika ngazi ya wadi.

Wananchi wenyewe kuamua

Kulingana na mswada huo, Hazina hiyo ya Maendeleo katika Wadi itatumiwa kufadhili miradi ambayo wananchi wenyewe wataamua.

“Mswada huo unaongozwa na haja ya kuhakikisha uwepo wa usawa kimaendeleo katika wadi; ambapo utahakikisha kuwa watu katika maeneo yaliyotengwa katika wadi wanapata miradi na huduma sawa na wenzao katika maeneo mengine.

Endapo mswada huo utapitishwa kuwa sheria, kila moja ya wadi 1,445 nchini itapokea angalau Sh10 milioni za maendeleo kutoka kwa bajeti ya maendeleo katika kila mojawapo ya kaunti 47 nchini.

Madiwani wamekuwa wakilalamika kuwa baadhi ya magavana huzinyima wadi fulani fedha za maendeleo kwa misingi kuwa wakazi wa huko hawakuwapigia kura kwa wingi katika chaguzi zilizopita.

“Ubaguzi kama huu, madiwani wanasema, huchangia baadhi ya maeneo wanayowakilisha kukosa kufikiwa na matunda ya ugatuzi,” akasema Bw Kang’ata.

  • Tags

You can share this post!

Spurs wapewa tiketi ya bwerere baada ya wanasoka 17 wa...

Msichana, 12, ndani kwa dai la kumuua mpenziwe