KICD yapata mkurugenzi mpya
Na CHARLES WASONGA
WAZIRI wa Elimu George Magoha amemteua mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Moi, Prof Charles Ong’ondo awe Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuandaa Mitaala Nchini (KICD) kwa kipindi cha miaka mitano.
Ong’ondo atachukua nafasi ya Dkt Joel Mabonga ambaye amekuwa akishikilia wadhifa huo kama kaimu baada ya Dkt Julius Jwan kuteuliwa kuwa Katibu katika Wizara ya Elimu anayesimamia idara ya Mafunzo ya Kiufundi na Kiteknolojia.
Dkt Mabonga ni naibu mkurugenzi mkuu wa KICD.
Prof Ong’ondo ni Profesa katika Taalumu ya Mafunzo ya Ualimu na Lugha ya Kiingereza katika Idara ya Mitaala na Mafunzo ya Uanahabari katika Chuo Kikuu cha Moi.
Prof Ong’ondo amefunza katika chuo kikuu cha Moi miaka 16 na ni baada ya kuhudumu kwa miaka kumi kama mwalimu wa shule za upili.
Tangu Juni 21, 2019, msomi huyo amekuwa mwanachama wa jopokazi kuhusu utekelezaji wa mageuzi ya mfumo wa elimu.
Sasa atakabiliana na kibarua kigumu cha kufanikisha utekelezaji wa mfumo mpya unaohusu Umilisi na Utendaji ambao ulivurugwa na janga la corona. Kisa cha kwanza cha Covid-19 kiliripotiwa nchini Machi 13, 2020.
Utekelezaji wa gredi ya tano ulipangiwa kuzinduliwa mwaka huu 2020 baada ya Wizara ya Elimu kufanikisha utekelezaji wa gredi 1, 2, 3, na 4.