• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
TAHARIRI: Kila mmoja asaidie kufufua upya utalii

TAHARIRI: Kila mmoja asaidie kufufua upya utalii

Na MHARIRI

LEO hii ulimwengu mzima unaadhimisha Siku ya Utalii Duniani, kwa kauli mbiu ‘kupeleka maendeleo mashambani’.

Umoja wa Mataifa (UN) umeteua mwito huu kama njia ya kuhimiza mataifa yazingatie zaidi maeneo ya kitamaduni pamoja na mila nzuri ambazo huenda, kutokana na watu kuangazia zaidi mijini, uzuri huo umesahauliwa au haujulikani.

Mapango makubwa, maporomoko ya maji, ngoma za kitamaduni na hata mavazi, ni baadhi ya mambo yanayopatikana mashambani.

Vivutio hivi si kwa ajili ya wageni kutoka nje ya Kenya pekee. Kuna Wakenya wengi ambao tangu wazaliwe hadi ukubwani mwao, hawajawahi kutembelea zaidi ya kaunti tano.

Bila ya kuchukua hatua na kujionea mambo ya kuvutia mashambani, itakuwa vigumu kwao kuelewa kuwa, tumebarikiwa nchi yenye vivutio vikubwa ulimwenguni.

Mwaka huu tunaadhimisha Siku ya Utalii Duniani tukiwa tumesambaratika kiuchumi kutokana na janga la Covid-19. Wakenya wa mijini na mashambani wanapitia hali sawa ya kukosa vyanzo vya pesa.

Punde tu baada ya kisa cha kwanza cha corona kutangazwa mwezi Machi, makampuni yalipunguza wafanyikazi.

Safari za ndege zilisimamishwa na hata biashara ndogo mashinani na mijini zikaathirika.

Kuendelea kupungua kwa visa vya maambukizi kunatoa fursa kwa nchi yetu kujipangusa vumbi na kuanza upya kuujenga uchumi. Hili halitakuwa jambo rahisi kama tunavyofikiria.

Hatua ya kwanza yafaa kuwa kuhimizana tuungane na kutembelea maeneo yaa kitalii.

Waziri wa Utalii, Najib Balala alipotoa taarifa kuhusu hali ya utalii mwezi Agosti, alionyesha kuanza kwa safari za ndege za kimataifa kumeanza kuwaleta wageni kutoka nje.

Lakini wageni hao hatuwezi kuwategemea sana wakati ambapo tisho la maambukizi ya corona haalijaondoka.

Kwa hivyo, jukumu kubwa sasa limo mikononi mwetu. Utalii huchangia aajira kwa vijana wengi, hasa wa mashambani ambao hujipatia riziki kwa kuongoza watalii, kucheza ngoma za kitaamaduni au kuwafasiria wageni kwa lugha zao.

Hali ya kawaida itaweza kurudi upesi tu iwapo Wakenya wote watajitolea na kuendeleza sekta ya utalii kwa pamoja.

Tunahitaji mikakati mizuei kutoka kwa wizara ya Utalii kama kupunguza malipo yaa milangoni kwenye mbuga. Lakini zaidi, huu ni muda mzuri kuyatangaza maeneo na tamaduni ambazo huenda shirika la Umoja wa Mataifa (Unesco) haalijayatambua.

You can share this post!

‘Handisheki’ itatupa Rais 2022 – Atwoli

Wachuuzi waendelea kukaidi marufuku ya plastiki