‘Handisheki’ itatupa Rais 2022 – Atwoli
Na SHABAN MAKOKHA
KATIBU mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi (Cotu), Bw Francis Atwoli, amesema kuwa mpango wa maridhiano (BBI) utaboresha uongozi nchini kwa kuibua mazingira bora ya uteuzi wa viongozi walio na mwelekeo halisi wakati wa uchaguzi mkuu wa 2020.
Mtetezi huyo wa haki za wafanyakazi alifichua kwamba muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Bw Raila Odinga ndio utakaotoa rais 2022.
“Atakayeteuliwa na handisheki ndiye atakuwa Rais wa Kenya mwaka wa 2022,” alisema Bw Atwoli.
Akizungumza wakati wa mazishi ya nduguye -Livingstone Ambetsa- katika shule ya msingi ya Mulwanda katika kaunti ndogo ya Khwisero jana, Bw Atwoli alimtaka Naibu Rais, Dkt William Ruto akome kuwapotosha Wakenya akiijiita “Hustler” yaani maskini, ilhali yeye si maskini.
“Maskini hawezi kumiliki ndege tano za helikopta, mashamba makubwa na mabilioni ya pesa katika akaunti zake. Tutamzima asiwe Rais kwa kutumia kila mbinu, kwa sababu amemzuia Kenyatta kutekeleza majukumu yake,” akasema Bw Atwoli.
Aliwatahadharisha Wakenya kwamba wakimchagua Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta watakuwa wamefanya makosa makubwa.
“Uongozi wa nchi hii utatoka kwa BBI. Hiyo ndiyo itakayohakikisha Wakenya wako na maisha mazuri,” akasema.
Aliongeza kusema kuwa BBI itatoa mwelekeo utakaowapa Wakenya matumaini mazuri siku za usoni.
Alisema, “BBI itateua rais na viongozi wengine katika kila pembe ya nchi hii.”
“Yafaa Dkt Ruto afahamu watu wenye ushawishi serikalini hawatamteua kuwania urais. Tutamfungia asipate uongozi wa nchi hii 2022,” akasema.
Bw Atwoli alitangaza mipango ya wazee wa eneo la Magharibi kufanya mkutano mkubwa katika uwanja wa Bukhungu mapema mwaka ujao, kuwatangaza viongozi wenye busara watakaochaguliwa katika nyadhifa mbalimbali 2022.
“Tutatengeneza orodha ya viongozi watakaochaguliwa kuanzia wadhifa wa Urais, Ugavana, Useneta na Wabunge pamoja na watu watakaokuwa wanazungumza kwa niaba ya eneo la Magharibi katika ngazi za kitaifa na wale watakaochaguliwa na maelfu ya wakazi wa eneo hili.”
Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017, Bw Atwoli alimtawaza kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi kuwa msemaji wa Jamii ya Waluhya ambapo pia Gavana Wycliffe Oparanya aliteuliwa kuwa naibu wa msemaji.”
Alisema wawaniaji viti ambao majina yao hayatakuwa katika orodha hiyo ya baraza la wazee watajilaumu wenyewe.