• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 11:34 AM
Sheffield United wakosa kupata alama wala bao katika mechi tatu za kwanza EPL

Sheffield United wakosa kupata alama wala bao katika mechi tatu za kwanza EPL

Na MASHIRIKA

LIMBUKENI wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Leeds United, walisubiri hadi dakika za mwisho kuwapokeza Sheffield United kichapo cha 1-0 kwenye gozi la Yorkshire lililochezewa ugani Bramall Lane mnamo Septemba 27, 2020.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa vikosi hivyo kukutana kwenye mechi ya EPL baada ya miaka 26.

Bao la pekee na la ushindi katika mechi hiyo lilifumwa wavuni na Patrick Bamford katika dakika ya 88. Goli hilo lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati ya Banford na Jack Harrison aliyemfanyisha kipa Aaron Ramsdale kazi ya ziada.

Matokeo ya mchuano huo yanawasaza Sheffield United bila alama wala bao lolote katika jumla ya mechi tatu za ufunguzi wa kivumbi cha EPL msimu huu.

Kikosi hicho kilipokezwa na Wolves kichapo cha 2-0 katika mechi ya kwanza ya ligi mnamo Septemba 14 uwanjani Bramall Lane kabla ya Burnley kuwabandua kwenye raundi ya pili ya Carabao Cup kwa mabao 5-4 kupitia penalti baada ya sare ya 1-1 mwishoni mwa dakika 90 mnamo Septemba 17.

Sheffield United waliomaliza kampeni za EPL mnamo 2019-20 katika nafasi ya tisa jedwalini kwa alama 54 sawa na Burnley, walipigwa 1-0 na Aston Villa katika mechi ya pili ya EPL muhula huu mnamo Septemba 21.

Majuto

Chini ya kocha Chris Wilder, Sheffield United watasalia kujutia nafasi nyingi walizopoteza baada ya John Lundstram kushindwa kumzidi maarifa kipa Illan Meslier mara tatu katika kipindi cha pili.

Leeds United ambao wanashiriki kivumbi cha EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 16, waliwapokeza Fulham kichapo cha 4-3 kwenye mchuano wao wa pili baada ya Liverpool kuwapepeta 4-3 katika mechi ya kwanza ugani Anfield.

Straika wa Leeds United Patrick Bamford (kulia) aruka kuugonga mpira kwa kichwa kufunga bao wakicheza dhidi ya Sheffield United uwanjani Bramall Lane mjini Sheffield, Septemba 27, 2020, ambapo Leeds imeshinda 1-0. Picha/ AFP

Mechi tatu za kwanza za Leeds United katika EPL muhula huu sasa zimeshuhudia jumla ya mabao 15 yakifumwa wavuni, hii ikiwa idadi ya juu zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu 1962-63. Msimu huo, Wolves walifunga mabao 12 nao wakaokota wavuni magoli mawili katika gozi la EPL.

Chini ya kocha Marcelo Bielsa, Leeds kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Manchester City, Wolves na Villa kwa usanjari huo. Kwa upande wao, Sheffield watapepetana na Arsenal, Fulham na Liverpool katika msururu wa michuano mitatu ijayo.

You can share this post!

Nitajituma kufa kupona hadi Harambee Stars waingie Kombe la...

Siku ya utalii duniani yaadhimishwa matumaini ya sekta...