Michezo

Olunga afunga bao na kuendeleza ubabe wake katika ligi kuu ya Japan

September 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI matata wa Harambee Stars, Michael Olunga aliendeleza ubabe wake katika soka ya Ligi Kuu ya Japan (J1-League) kwa kufunga bao katika mechi iliyoshuhudia waajiri wake Kashiwa Reysol wakipokezwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa Yookohama Marinos.

Hadi alipowajibishwa katika gozi hilo, mfumaji huyo wa zamani wa Gor Mahia hakuwa amewafungia Reysol goli lolote katika mechi mbili.

Akicheza dhidi ya Yokohama, aliwaweka waajiri wake kifua mbele kunako dakika ya 40 kwa kukamilisha kwa kichwa mpira wa kona.

Hata hivyo, Yokohama walirejea mchezoni kwa matao ya juu katika kipindi cha pili na kusawazisha mambo katika dakika ya 77 kupitia kwa Erik Lima kabla ya Takuma Ominami wa Reysol kujifunga na kufanya mambo kuwa 2-1 kwa upande wa Yokohama.

Daizen Maeda ndiye zliyezamisha kabisa chombo cha Resyol kwa kuwafunga bao la tatu lililowazamisha wapinzani kabisa mwishoni mwa kipindi cha pili.

Kushindwa kwa Reysol kulishusha hadi nafasi ya nane kwenye jedwali la vikosi 18. Kikosi hicho kwa sasa kinajivunia alama 30 kutokana na mechi 19 za hadi kufikia sasa.

Kwa upande wao, Yokohama walipaa hadi nafasi ya 13 kwa alama 20 kutokana na mechi 19 ambazo wamezisakata hadi kufikia sasa muhula huu.

Olunga anatazamia sasa kuwajibishwa tena katika mechi ijayo ambayo itawakutanisha Reysol na Yokohama FC mnamo Oktoba 3, 2020.

Licha ya kujivunia rekodi nzuri, Olunga hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na Stars katika mechi nne zijazo zikiwemo mbili dhidi ya Comoros katika juhudi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zitakazoandaliwa Cameroon mnamo 2021.

Chini ya kocha Francis Kimanzi, Stars wamepangiwa kuvaana na Comoros katika mkondo wa kwanza jijini Nairobi mnamo Novemba 9 kabla ya kurudiana na kikosi hicho jijini Moroni siku nne baadaye.

Kabla ya kupigwa kwa mechi hizo za mikondo miwili dhidi ya Comoros katika Kundi G linalojumuisha pia Togo na Misri, Stars wameratibiwa kupimana nguvu na Zambia na Sudan mnamo Oktoba 2020.

Ingawa hivyo, Kashiwa Reysol wanaojivunia huduma za Olunga katika Ligi Kuu ya Japan (J1-League), wamethibitisha kwamba hawatamwachilia fowadi huyo kurejea Kenya kuwajibikia Stars kwa sasa.

Iwapo atatua humu nchini kuchezea Stars, Olunga atalazimika sasa kukosa jumla ya michuano saba ya Kashiwa kwa sababu ya kanuni za afya zinazodhibiti msambao wa ugonjwa wa Covid-19.