Mutunga ajiunga na vuguvugu jipya la kisiasa
Na CHARLES WASONGA
WANAHARAKATI nchini wamezindua vuguvugu la kisiasa ambalo wanatarajia kutumia kupigania uongozi bora wa nchi.
Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa vuguvugu la Kongamano la Mageuzi (KLM), aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga, alipinga mageuzi ya katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI) na kuhimiza utekelezaji wake huku akipendekeza kuondolewa mamlakani kwa viongozi wote wa sasa.
Dkt Mutunga alisema changamoto kuu nchini wakati huu ni uongozi mbaya wa kisiasa.
“Nakubaliana na wakereketwa wa KLM kwamba BBI ni mradi wa kundi la wanasiasa ambao lengo lao kuu ni kutwaa mamlaka ya serikali na nchi kwa manufaa yao. Hii ndio maana napinga shinikizo za mageuzi ya katiba yanayolenga kutimiza azma hii,” akasema katika ukumbi wa jumba la Ufungamano, Nairobi.
Dkt Mutunga alisema utekelezaji Katiba kikamilifu ndio utawezesha Wakenya kupata bidhaa na huduma wanazohitaji kuendeleza maisha yao wakati huu ambapo wanakabiliwa na changamoto si haba zilizosababishwa na janga la Covid-19.
“Wakenya wanataka kuishi katika mazingira ambapo wanapata kwa gharama nafuu, mahitaji kama vile elimu, afya, nyumba, maji, kawi, uchukuzi, chakula, ardhi, usalama na haki,” akaeleza. Dkt Mutunga alisema viongozi wote walioko serikalini na wale wa upinzani wamewahi kutoa ahadi nyingi hapo awali ila wameshindwa kuzitimiza kwa sababu wengi wao wanaongozwa na ukabila “ambao ndio umezaa ufisadi.”
“Hawa viongozi wa sasa ni zao la viongozi wa nyuma ambao kwa pamoja wameshindwa kuleta mabadiliko bora kwa miaka 57 iliyopita. Kwa mara nyingine wakati wa janga la corona wameshindwa kuwasaidia wananchi huku wandani wao wakipora fedha za kukabiliana na tatizo hilo la kiafya,” akasema.
Dkt Mutunga aliandamana na mwasisi wa vuguvugu la KLM, mwanaharakati John Githongo. Bw Githongo alisema vuguvugu hilo linapanga kudhamini wagombeaji katika nyadhifa zote sita, kuanzia urais hadi udiwani, katika uchaguzi mkuu wa 2022.