Chuo Kikuu cha Eldoret chaanza utafiti wa tiba asili ya Covid-19

Na DENNIS LUBANGA

VITA dhidi ya virusi vya corona vimepigwa jeki baada ya Chuo Kikuu cha Eldoret kuimarisha harakati zake za kubaini ikiwa dawa za kiasili zina uwezo wa kudhibiti ugonjwa huo na mengine sugu.

Dkt Mark Kiptui, ambaye anaongoza mpango wa ushirikiano katika ya chuo hicho na madaktari wa tiba za kiasili kutoka eneo la North Rift, Jumamosi alitembelea kliniki ya Tana Herbal mjini Edoret ambako alichukua sampuli za dawa za kiasili zitakazopimwa katika maabara yao.

Haya yanajiri siku kadhaa baada ya Chuo Kikuu cha Eldoret kufichua kuwa kimetia saini Mkataba wa Maelewano (MoU) na Chama cha Matabibu wa Kiasili kutoka North Rift kuhusiana na utafiti wanaouendesha kusaka dawa ya Covid-19.

Mmiliki wa kliniki hiyo ni Jamal Mungatana Diriwo Omar, tabibu anayetumia dawa za kiasili na ambaye amedai kugundua tiba ya Covid-19.

“Nimetembelea kliniki ya Dkt Mungatana kukusanya sampuli za dawa zake ili kuweza kuzifanyia utafiti zaidi kubaini ikiwa zina uwezo wa kutibu Covid-19 na magonjwa mengine kama vile kansa,” Dkt Kiptui akaeleza.

Taifa Leo iligundua kuwa chuo hicho kinaendelea kukamilisha MoU nyingine na kliniki hiyo ili kuimarisha ushirikiano kati yao.

Kulingana na Dkt Mungatana, chuo hicho kilichukua sampuli tatu kutoka kwa kliniki yake, ambazo ni The Great 9 Antivirus, Q-Al-Hindi na Al-Hurfu.

“Dkt Kiptui alitutembelea na tukampa dawa za kienyeji ambazo tunaamini kuwa kupitia usaidizi kutoka kwao, zitatoa suluhu kwa janga hili na magonjwa mengine sugu nchini na kimataifa ili hali ya kawaida irejee,” akasema Dkt Mungatana ambaye aliongeza kuwa ana tajriba ya zaidi ya miaka 20 katika sekta ya tiba za kiasili.

Akaongeza, “Dawa aina ya The Great 9 antivirus hutibu aina zote za saratani, Q-Al-Hindi hutibu nyumonia (kichomi) na kusafisha mapafu huku Al-Hurfu ikiwa na uwezo wa kudhibiti kuongezeka kwa aina zote za virusi huku ikisafisha mapafu na mishipa ya kupumua.

Mnamo Mei mwaka huu, Chuo Kikuu cha Eldoret kupitia Naibu Chansela Prof Teresia Akenga kilitangaza kuwa kiko tayari kushirikiana na madaktari wanaotibu kwa kutumia dawa za kiasili kuendesha tafiti kubaini ikiwa dawa hizo zina uwezo wa kupambana na Covid-19.

Awali, Dkt Mungatana alikuwa amewasilisha pendekezo kwa chuo hicho, akitoa ithibati kuwa dawa zake za kiasili zina uwezo wa kutibu Covid-19, ugonjwa ambao umevuruga maisha ulimwenguni kote.

Dkt Kiptui aliongeza kuwa serikali imekubali matumizi ya dawa za kiasili baada ya kuona kazi nzuri inayofanywa na madaktari wa kiasili katika kutibu maradha mbalimbali.

Habari zinazohusiana na hii