Habari Mseto

EACC na Maseneta walumbana kuhusu uchunguzi wa ufisadi katika Wizara ya Afya

September 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MAJIBIZANO makali yalizuka kati ya maafisa wakuu wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na maseneta kuhusiana na uchunguzi kuhusu sakata ya ununuzi wa kliniki tamba za konteina ambazo hazijatumika kwa miaka minne.

Wanachama wa kamati ya Seneti kuhusu Afya walimshambulia Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Twalib Mbarak alipokosa kutoa maelezo kuhusu uchunguzi kuhusu sakata hiyo.

Maseneta Ledama Ole Kina (Narok), Abdullahi Ali (Wajir) na Mary Seneta (seneta maalum) walitaka maelezo zaidi kuhusu sakata hiyo kama vile majina ya kampuni kumi zilizopigania zabuni ya kuwasilisha kampuni zilizoshindania zabuni ya kuwasilisha konteina hizo na wakurugenzi wazo.

Hata hivyo, Bw Mbarak alikataa, akisema kufichua maelezo hayo kutaathiri uchunguzi ambao ungali unaendelea kuhusu mradi huo. Mradi huo maarufu kama, “Special Portable Clinics Project, ulianzishwa na Serikali ya Kitaifa mnamo 2015 kwa lengo la kusambaza kliniki tamba katika mitaa ya mabanda katika maeneo ya miji.

“Sitetei mtu yeyote lakini siwezi kutoa maelezo ambayo mnataka. Hatuwezi kutoa masuala ya ndani kuhusu suala hilo kwani hatua hiyo itavuruga uchunguzi ambao bado unaendelea,” akawaambia maseneta hao.

Wanachama wa kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Trans Nzoia Michael Mbitho walikuwa wametaka maelezo ya kina kuhusu kampuni 10 zilizoalikwa na Wizara ya Afya kuwania zabuni kuhusu mradi huo.

“Tunataka kujua ikiwa sheria ilizingatia kuchagua kampuni hizo 10,” akasisitiza Dkt Mbito.

Hayo yanajiri baada ya EACC kuwasilisha stakabadhi mahakamani ikionyesha kuwa ina ushahidi kuonyesha kuwa maafisa katika Wizara ya Afya walishirikiana na kampuni fulani kuongesha gharama ya kliniki hizo tamba kutoka Sh308 milioni hadi Sh800 milioni.

EACC iligundua kuwa konteina hizo zilizoundwa kuwa kliniki tamba ambayo zingegharimu Sh3 milioni kila moja uliuziwa Wizara ya Afya kwa Sh10 milioni kila moja na kampuni moja ya China.

Uchunguzi ulionyesha jkuwa kampuni hiyo kwa jina Guangzhuo Moneybox Steel Structure Ltd, ilipokea Sh525 milioni kutoka kwa kampuni ya Estama Investment Ltd ilipewa zabuni na Wizara ya Afya. Hii ina maana kuwa kampuni hiyo ya Estama ilitia kibindoni Sh275 milioni kwa kuwa wakala tu.

Wakati wa sakata hiyo, Katiba katika Wizara ya Ardhi Nicholas Muraguri ndiye alikuwa Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu Nchini. Katibu katika Wizara ya Afya alikuwa Bi Khadijah Kassachon.

Tangu Novemba 3, 2016, EACC imekuwa ikichunguza madai ya ukiukaji wa sheria katika utoaji wa zabuni kwa kampuni ya Estama Investment Ltd ya kuwasilisha kliniki tamba 100 kwa gharama ya Sh10 milioni kwa kila moja. Kwa ujumla mradi huo ulitarajiwa kugharimu Sh1 bilioni.

Bw Mbarak aliambia kamati hiyo ya Seneti kuhusu Afya kwamba walipata stakabadhi kutoka kwa Wizara ya Afya, benki mbali mbali, Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) na Msajili wa Kampuni. Pia wameweza kuandikisha taarifa kutoka kwa watu 58 kuhusiana na sakata hiyo.

Alikuwa ameandamana na Mkuu wa Uchunguzi katika EACC Abdi Ahmed.

Mwishowe, Bw Mbarak alisalimu amri kutokana  na presha kutoka kwa maseneta wanachama wa kamati hiyo, akiwemo Seneta wa Wajir Abdullahi Ali, na akakubalia kufichua maelezo hayo mradi “maseneta wasiyafichue kwa umma.”