• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Sina nia ya kumkaidi Uhuru, Ruto sasa ajitetea

Sina nia ya kumkaidi Uhuru, Ruto sasa ajitetea

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU Rais William Ruto amepuuzilia mbali shinikizo za kumtaka kujiuzulu kutokana na madai kwamba anamkaidi Rais Uhuru Kenyatta.

Dkt Ruto jana alisema kuwa, Rais Kenyatta ameridhishwa na utendakazi wake na amekuwa akitekeleza majukumu yote anayopewa na mkubwa wake.

Kulingana naye, Rais hajawahi kulalamikia utendakazi wake.

“Rais Kenyatta hajawahi kunipa kazi nikakosa kuifanya. Kila kazi ninayopewa nimeitekeleza kwa ustadi,” akasema Dkt Ruto aliyekuwa akihutubia kundi la wanawake wafanyabiashara waliomtembelea nyumbani kwake mtaani Karen, Nairobi.

Wakosoaji wa Dkt Ruto wamekuwa wakimshinikiza kujiuzulu huku wakisema kuwa hajakuwa akitekeleza majukumu yoyote serikalini.

Tukio la hivi karibuni zaidi lililoonekana kuwa la ukaidi ni alipokosa kuhudhuria kongamano la kitaifa kuhusu Covid-19 licha ya kualikwa na kuthibitisha angehudhuria, jina lake likajumuishwa kwenye ratiba ya wale waliotakiwa kuhutubu.

Katika kongamano hilo la Jumatatu, ilibidi Waziri wa Usalama wa Nchi, Dkt Fred Matiang’i kutwaa jukumu la kumwalika Rais kuhutubia taifa. Dkt Ruto ndiye alikuwa ameratibiwa kutekeleza wajibu huo.

Wanasiasa wanaoegemea upande wa Rais Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga walimtaka Dkt Ruto kujiuzulu kwa ‘kukaidi’ Rais Kenyatta.

Wanasema kukosa kwa Naibu wa Rais katika kongamano ilikuwa ishara ya ukaidi na kumdharau Rais Kenyatta.

“Wanaojifanya kuwa wasimamizi wangu waelekeze juhudi zao katika kuwahudumua wananchi. Wao ni akina nani kulalamikia utendakazi wangu? Nani aliwafanya kuwa wasimamizi wangu? Ninajua kazi yangu vyema na bosi wangu (Rais Kenyatta) hajalalamika,” akasema Naibu wa Rais jana.

Naibu mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe ni miongoni mwa viongozi wa chama tawala waliomtaka Dkt Ruto kujiuzulu kwa kukosa kuhudhuria kongamano la Covid-19.

Mbunge wa Kiambaa, Paul Koinange, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Bungeni, alimtaka Dkt Ruto kujiuzulu iwapo anahisi kutoridhishwa na serikali ya Rais Kenyatta.

Mbunge wa Kieni Kanini Kega ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Bungeni alipendekeza Dkt Ruto kuadhibiwa kwa kukaidi Rais Kenyatta.

Mara ya mwisho kwa Dkt Ruto kukutana na Rais Kenyatta ilikuwa Septemba 10, ambapo walihudhuria kikao cha Baraza la Mawaziri kwa dakika chache na kisha Naibu wa Rais akasafiri hadi katika Kaunti ya Kisii kuongoza hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya wahudumu wa bodaboda.

You can share this post!

Zaidi ya vyama 400 kumenyania kura za 2022

Amina Abdalla: Tegemeo la watu wenye akili punguani Mombasa