Makala

Amina Abdalla: Tegemeo la watu wenye akili punguani Mombasa

October 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 4

Na DIANA MUTHEU

“KILA ‘mwendawazimu’ ana historia ndefu ya mambo yaliyopelekea hali yake,” anasema Bi Amina Abdalla, mwanamke ngangari kutoka kaunti ya Mombasa ambaye amejitolea kuwatunza na kuwajali wagonjwa wa akili, kupitia shirika lake la Women Empowerment Network.

Kwa miaka tisa sasa, Bi Amina amekuwa akizunguka katika mitaa tofauti katika kaunti hiyo, akiwakusanya wagonjwa hao na kuwapeleka katika kituo spesheli cha kuwahudumia cha Portreitz, Mombasa.

Pia, amekuwa akijitolea kugharamia matibabu yao, na baadhi yao wamepona na kurejeshwa makwao ambapo wengine walitokea sehemu kama vile Garissa, Somalia, Thika, Kwale, Kilifi, Machakos miongoni mwa sehemu zingine.

Anasema kuwa swala la kuwaona wagonjwa hao wakiishi bila hadhi yoyote mitaani, wakila vya pipani na kuogopwa na wanajamii, aliamua kuwa tegemeo lao.

“Nilianza programu hii mwaka wa 2011 kwa kuwa niliwaona watu hao wakiwa barabarani wakirandaranda ovyo bila chakula na maji. Baadhi ya wanawake walikuwa wanatembea uchi, jambo ambalo ni la kuabisha. Nilijiuliza ni mambo mangapi yanawakumba wagonjwa hao haswa wanawake hao na nikaamua kutafuta suluhu,” akasema Amina ambaye ni mkurugenzi katika shirika la Coast Development Authority.

Akisimulia safari yake katika programu hii kwa Taifa Leo Dijitali, Amina alisema kuwa mara ya kwanza kabisa kuianza programu ile, aliwakusanya wagonjwa wa akili saba na kuwapeleka katika kituo hicho cha Portreitz.

Zaidi, alinunua magodoro, vyakula na vitu vingine muhimu ambavyo wangehitaji pale, ndipo wagonjwa hao wakakubaliwa katika hospitali hiyo.

“Sikutaka wagonjwa hao waonekane kama mzigo kwa wahudumu katika hospitali hiyo, na nilichukua jukumu la kuhakikisha wanapata kila kitu walichohitaji,” akasema.

Bi Amina Abdalla akizungumza na waandishi wa habari katika Chuo Anwai cha Kenya, Mombasa. PICHA/ DIANA MUTHEU

Hata hivyo, anasema kuwa watu wengi hawakuwa na imani kuwa angeiweza kazi hiyo.

“Watu wengi waliniambia kuwa sitaiweza kazi hiyo lakini sikuwasikiliza kwani nilikuwa nimeandaa roho yangu kujitosa katika programu hiyo. Wengine walisema kuwa naendeleza siasa zangu kupitia programu hiyo lakini sikuwasikiliza kamwe,” akasema Amina.

Amina alisema kuwa baada ya miezi sita, miongoni mwa wagonjwa hao saba, wanne walipona na aliwarejesha makwao na kuwaanzishia biashara zao.

Hata hivyo, alisema kuwa alipata changamoto kwani baadhi ya wagonjwa waliopona na kurejeshwa nyumbani walirudi katika hali yao ya hapo awali, kwa sababu familia zao hazikufuata maagizo ya kuwapa lishe bora na dawa kwa wakati ufaao.

Lakini, hakufa moyo bali alijaribu tena na hadi wa leo wagonjwa 95 wameweza kufaidika kupitia shirika lake.

“Ili wagonjwa hawa wapone haraka, wanahitaji kuonyeshwa upendo, kutunzwa na pia wanaowahudumia wawe na subira,” akasema.

Kwa kawaida, gumzo mtaani ni kuwa wagonjwa wengi wa akili ni watu ambao walifanya jambo mbaya, ndipo wakaweza kufanyiwa uganga au ushirikina wa aina tofauti.

Kulingana na Bi Amina, hali hiyo ni ugonjwa kama vile magonjwa ya kawaida, na inaweza kutibiwa na mtu akarejea katika hali yake ya kawaida.

Alitaja baadhi ya sababu zinazopelekea mgonjwa kupata maradhi hayo kama kusongwa na mawazo na matumizi ya dawa za kulevya kupita kiasi.

“Mmoja wa wagonjwa ambaye nishawahi kumhudumia alikuwa ni daktari ambaye alisongwa na mawazo baada ya mipango yake ya kuendeleza masomo yake nchini Cairo iliambulia patupu na mwingine ni mzee aliyetengana na mkewe ambaye walikuwa katika ndoa kwa muda mrefu” akasema.

Mwaka huu mnamo Februari, Amina aliamua kutafuta makazi ambapo wagonjwa hao watashughulikiwa vilivyo kwa muda mrefu.

“Kuna wagonjwa tumekuwa tukiwahudumia kwa miaka miwili, na wanaendelea vizuri kiafya. Watu hawa wanahitaji matibabu, kuonyeshwa upendo, kupewa ushauri kwa muda mrefu, ili waweze kupona kikamilifu. Pia, wanahitaji kukubaliwa katika jamii,” akasema Bi Amina.

Janga la corona lilipoikumba nchi yetu, Bi Amina alijitahidi kuwasaidia wagonjwa 55 wa akili manake serikali ilikuwa imewatenga katika miradi yao ya kutoa vyakula vya msaada, barakoa n ahata vifaa vingine vya kudumiasha usafi kama vile sabuni na maji safi.

Bi Amina aliwatafutia wagonjwa hao maeneo salama katika Chuo Anwai cha Kenya, Mombasa, na hata kuiomba kaunti iwapime kuthibitisha iwapo walikuwa na corona.

Hii ni kwa sababu wengi wao walikuwa wamechukuliwa kutoka eneo la Old Town, ambapo marufuku ya kuingia na kutoka ilikuwa imetangazwa na Rais Uhuru Kenyatta kwa kuwa watu wengi pale walikuwa wameambukizwa virusi vya corona.

Watano kati ya wagonjwa hao walipatwa na maradhi ya Covid-19, ikiwemo mzee mmoja mwenye miaka 85.

Aliongeza kuwa wagonjwa wengi wa akili ambao amewahi kuwahudumia katika programu hiyo huwa kati ya miaka 29 na zaidi.

“Tulishirikiana na kaunti na nilipata madaktari, wauguzi na dawa. Wagonjwa hao walikuwa wanawekwa katika vyumba tofauti punde tu walipofika katika kituo hicho,hadi pale daktari alisema kuwa wako salama kujumuika na wenzao. Waliopatikana na virusi vya corona walitengwa hadi pale walipopona,” akasema Bi Amina.

Baada ya tangazo kutolewa kuwa shule zingefunguliwa, Bi Amina aliwahamisha wagonjwa wale hadi eneo la Shanzu ambapo wanatunzwa na wafanyikazi nane ambao wamejifunza kuishi nao kadri wanapoendelea kuwahudumia, pamoja na vijana wanne waliojitolea baada ya kupona maradhi ya akili.

“Vijana hao hutusaidia kuwalisha, kuwaogesha, kuwapa dawa na hata kucheza na wagonjwa,” akasema Bi Amina huku akieleza kuwa kuwatunza wagonjwa hawa nyumbani ndilo jambo muhimu zaidi.

“Wagonjwa wengi waliopona tuliwaregesha makwao, wengine sita watapata mafunzo ya kinyozi na kusafisha magari na watakapohitimu, tutawafungulia biashara hizo,” akasema.

Amina alisema kuwa anawategemea marafiki na wafadhili kuendeleza programu hiyo. Aliongeza kuwa kila mwezi anatumia Sh350,000 kugharamia kodi ya nyumba, chakula, dawa na mahitaji mengine ya wagonjwa hao.

“Familia yangu imekubali kuwa wagonjwa hawa wanatuhitaji. Mara ya kwanza nilipata changamoto kwa kuwa nilijishughulisha na wagonjwa mara kwa mara na wagonjwa hao, na kukaa na familia kwa muda mfupi tu. Kufikia leo, watoto wangu huja katika makazi ya wagonjwa wale, wakawalisha na kuwapa dawa,” akasema.

Bi Amina anasema kuwa angependa jamii iwache tabia ya kuwatenga wagonjwa hao na kufahamu kuwa maradhi ya akili yanaweza kutibiwa na mtu akapona.

“Pia, nawaomba wawe mstari wa mbele kuwakamata wagonjwa hawa na kuwapeleka hospitalini. Pia, ningeomba serikali itenge fedha kwa mashirika yanayowasaidia wagonjwa hao,” akasema Bi Amina.

Alisema kuwa tayari wametafuta ardhi eneo la Miritini ambapo watajenga makazi ya watu wenye maradhi ya akili ambapo wagonjwa 100 wanaweza kutunzwa.

“Tunaomba wasamaria wema wajitokeze na kusaidia programu yetu,” akasema huku akiongeza kuwa kuwasaidia wagonjwa wa akili kumemfundisha asiwe mwepesi wa kuhukumu, kila binadamu ana haki na pia imemfunza kuwa mvumilivu.