Zani akataa kuunga mkono Boga, asema amemchoka
Na MOHAMED AHMED
UHASAMA wa kisiasa baina ya wanachama wa ODM waliowania tiketi ya chama hicho kwenye mchujo wa kuwania ubunge katika uchaguzi mdogo wa eneo la Msambweni, unaonekana kuendelea hata baada ya shughuli hiyo kukamilika.
Uwaniaji wa tiketi hiyo kati ya Bw Omar Boga na Nicholas Zani ulikamilika mnamo Alhamisi jioni ambapo Bw Boga alishinda uchaguzi huo mdogo wa chama.
Bw Boga alizoa kura 6,183 na kumshinda kwa mbali sana Bw Zani ambaye alipata kura 530 pekee kutoka kwenye vituo 60 vilivyotumika.
Hata hivyo, hata baada ya matokeo kuonyesha mshindi wazi kwenye mchujo, Bw Zani ambaye ni nduguye Seneta Maalum Dkt Agnes Zani, ameonekana kutokuwa na msimamo wa iwapo ataunga mkono chama chake kwenye uchaguzi huo unaopangwa kufanyika Disemba 15.
Hii ni licha ya Bw Boga kutoa wito kwa msindani wake huyo amuunge mkono ili waweze kushinda kiti hicho kama chama.
“Mimi wito wangu katika kampeni zangu ni kuwa siwachi mtu nyuma. Kwa hivyo nimesema wale wote ambao wapo kwenye chama, tuungane ili tuweze kuleta ushindi,” akasema Bw Boga kwa njia ya simu.
Akizungumza baada ya ushindi wake, alisisitiza kuwa tangu awali, yeye alitambua kuwa hakuwa anapigania tiketi hiyo dhidi ya Bw Zani, bali vita vyake vilikuwa baina yake na watu aliowataja kutoka kundi la Tangatanga.
“Hata wale wasimamizi wa mshindani wangu walikuwa ni watu ambao tunawajua. Sio wa ODM bali wa upande ule mwengine. Lakini mimi nasema hayo yamepita na hata hao watu wa Tangatanga bado tutawashinda,” akasema.
Kwa upande wake, Bw Zani alikuwa ameweka wazi kuwa hatomuunga mkono Bw Boga akisema kuwa amefanya hilo kwa muda sasa.
“Nimemuunga mkono sana Bw Boga na sasa imetosha. Nimepitia mengi hapo wakati wa nyuma na sasa ni basi,” alisema Bw Zani wakati alipopiga kura yake mnamo Alhamisi.
Jana, Taifa Leo ilipomuuliza tena kuhusiana na swali hilo, Bw Zani alikosa kujibu na badala yake alisema kuwa atatoa taarifa kwa bodi ya uchaguzi wa chama.
“Nitatoa uamuzi wangu kuhusiana na uchaguzi ujao kwa NEB na nitaongea na wale wanaoniunga mkono hivi karibuni,” alisema Bw Zani katika ujumbe mfupi aliyotuma kwa mwandishi wetu.
Hivi tofauti hizo zikeonekana bado zingalipo, hali hii inaweza kutatiza kampeni za chama cha ODM kinapoelekea kwenye uchaguzi huo mdogo. Hata hivyo, ufuasi wa Bw Zani unaonekana kuwa mdogo mno kulingana na kura kidogo alizopata juzi.
Kwa sasa, ni wazi kuwa Bw Boga atapambana na Feisal Bader ambaye anafadhiliwa na Naibu Rais William Ruto kwenye kinyang’anyiro hicho kinachosubiriwa kwa hamu.
Wawaniaji wengine wa kiti hicho ni Bi Mariam Sharlet ambaye ni mgombeaji huru na wengine ni Shee Abdulrahman (Wiper) na Bw Liganje Mwakaonje wa chama cha United Green Movement.