• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Uhuru asema uongozi wake unawajumuisha wanawake

Uhuru asema uongozi wake unawajumuisha wanawake

Na CECIL ODONGO

RAIS Uhuru Kenyatta amesema kwamba utawala wake bado unalenga kuhakikisha kwamba kuna usawa wa kijinsia na wanawake wanajumuishwa kwenye masuala ya uongozi nchi.

Kiongozi wa nchi alisema serikali ya Jubilee imeweka sera na asasi muhimu kuhakikisha kwamba wanawake hawaachwi nje kwenye masuala ya kitaifa pamoja na kuwekeza kwenye miradi ya kuwainua.

“Kenya ilikuwa mwenyeji wa Kongamano maarufu la wanawake mnamo 1985. Wakati wa Kongamano hilo, taifa letu lilitoa mwongoza ambao umekumbatiwa kuhakikisha kwamba miradi ya kuwainua wanawake inakumbatiwa,” akasema Rais Kenyatta.

Aidha, Rais alisema utawala wake umefanikiwa kupiga hatua kubwa katika kumaliza dhuluma za kijinsia hasa dhidi ya wanawake na wasichana. Baadhi ya dhuluma hizo ni kupigana na ukeketaji na kuhakikisha wasichana wote hasa kutoka jamii zenye tamaduni potuvu wanapata elimu.

“Utawala wangu umekuwa katika mstari wa mbele kupigana na tamaduni zisizofaa na dhuluma dhidi ya wanawake. Tayari tumeanza kuelimisha jamii zinazoshiriki ukeketaji kama njia ya kudhihirisha kuwa wasichana wamekomaa kwamba kuna njia nyinginezo za kuonyesha wanawake wamebaleghe,” akaongeza.

Rais Uhuru Kenyatta alikuwa akizungumza wakati wa Kongamano la 25 kuhusu wanawake duniani lililoandaliwa nchini Ufaransa na kuhusu wanachama wa Baraza la Umoja wa Kimataifa (UN).

Alisisitiza kwamba Kenya imekuwa ikishirikiana na majirani zake kama Tanzania, Somalia na Ethiopia na hata kusaini mkataba wa kumaliza ukeketaji hasa katika makabila yanayoishi kwenye mipaka ya nchi hizo tatu.

Kauli ya Rais inajiri wakati ambapo Jaji Mkuu David Maraga alimrai avunje mabunge ya Seneti na lile la Kitaifa kwa kukosa kupitisha sheria iliyoko kwenye katiba ambayo inaamrisha wanawake washikilie theluthi mbili ya nafasi zote za uongozi nchini.

Vilevile, Rais alieleza kongamano hilo jinsi ambavyo Kenya imekuwa ikiendeleza vita dhidi ya janga la virusi vya corona ambalo limeathiri mataifa mengi duniani na kusababisha vifo vya raia.

“Utawala wangu ulichukua hatua ya dharura na kuweka sera madhubuti ili kupigana na janga hili la virusi vya corona. Pia tulianzisha sera za kuwainua raia kiuchumi ikizingatiwa wengi walipoteza ajira. Hii ni kupitia kuanzisha hazina ambayo pia imekuwa ikitumika kufanikisha vita dhidi ya corona,” akasema.

You can share this post!

UTEUZI WA WANAJESHI SERIKALINI WAZUA KIWEWE

Wimbi katika jahazi la UhuRuto latikisa nchi