Kimataifa

Trump afutilia mbali safari za kampeni baada ya kuugua corona

October 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na AFP
BAADA ya kupuuza na kutania kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona kwa muda, hatimaye Rais Donald Trump ametangaza kuwa yeye na mkewe Melania wamethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo hatari.

Tangazo hilo litamfanya akose kushiriki kampeni za urais ambao utafanyika siku 31 zijazo.

Madaktari wake walisema rais huyo mwenye umri wa miaka 74, anahisi vyema na ataendelea kutekeleza majukumu yake akiwa amejitenga katika Ikulu ya White House.

Rais huyo alitangaza kupitia ujumbe wa Twitter kwamba yeye na mkewe Melania Melania Trump, 50, waliambukizwa virusi hivyo.

Kufuatia tangazo hilo, Trump alilazimika kufutilia mbali safari za kampeni, hatua ambayo inaweza kuathiri vibaya umaarufu wake ambao umekuwa ukishuka.

Kura za maoni zimekuwa zikionyesha mpinzani wake wa chama cha Democratic, Joe Biden akiwa kifua mbele kwa umaarufu.

Biden amekuwa akilaumu Trump kwa kutojitolea kikamilifu kukabiliana na janga hilo na kupuuza hatari ya virusi hivyo.

Trump amekuwa akihudhuria mikutano ya kampeni yenye misongamano ya watu kote nchini humo.

Mikutano hiyo ambayo anasema inadhihirisha nguvu zake za kisiasa, huwa inavutia maelfu ya watu, wengi wasiovalia barakoa na kutozingatia kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.

Mbinu hii sasa huenda ikasambaratika huku ikulu ya White House ikifutilia mbali mkutano wa kampeni uliopangwa katika jimbo la Florida jana.

Ilikuwa wazi kwamba Trump pia atafuta ziara aliyopanga Wisconsin mwishoni wikendi hii.

Pia alitarajiwa kusafiri sana wiki ijayo zikiwemo safari ndefu katika majimbo yaliyo magharibi mwa Amerika.

Huenda pia akakosa mjadala wa pili wa wagombea urais kati yake na Biden ambao umepangwa kufanyika Oktoba 15.

Akiwa na umri wa zaidi ya miaka 70 na mwenye mwili mnene, Trump yuko katika kundi la watu walio katika hatari ya kuathiriwa zaidi na makali ya corona.

Daktari wake rasmi, Sean Conley, alisema kwenye taarifa kwamba rais huyo na mkewe wako hawako kwenye hatari kwa wakati huu.

“Wanapanga kukaa nyumbani katika White House wakati huu,” alisema.

“Hata hivyo, ninatarajia rais ataendelea kutekeleza majukumu yake bila kutatizika anapoendelea kupata nafuu,” aliongeza.

Habari za kuugua kwa Trump zilijiri baada ya mmoja wa washauri wake wa karibu, Hope Hicks, kuripotiwa kuambukizwa virusi hivyo.

Hicks, 31, alikuwa ameandamana na Trump eneo la Cleveland kwa mjadala wake wa kwanza na Biden mnamo Jumanne. Alikuwa naye pia katika mkutano wa kampeni Minnesota mnamo Jumatano.