• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:55 PM
AWINO: Wakulima hawana cha kujifutia jasho, wanapunjwa tu

AWINO: Wakulima hawana cha kujifutia jasho, wanapunjwa tu

NA AG AWINO

Mapema mwezi jana, polisi walinasa tani nyingi za mchele ulioharibika ambao ulikuwa umepangiwa kuuzwa nchini. Ulikuwa wa thamani ya mamilioni ya pesa.

Shehena hiyo kubwa ilipangiwa kuuzwa kwa bei ya chini kuliko mchele unaokuzwa Mwea na maeneo mengine nchini. Duru zasema mchele huo ulikuwa umeagizwa kutoka mataifa ya Pakistan na Thailand.

Isitoshe, ilidaiwa mchele huo umeongezwa kemikali inayoipa harufu ya kuvutia na kuufanya mnunuzi awe na hamu ya kuula licha ya hatari zilizopo kwa afya yao.

Vile vile, kumekuwea na tetesi kuhusu ubora wa mchele unaotoka nchi za nje ambazo hazitimizi viwango vya ubora vinavyohitajika.

Yamkini bei ya bidhaa hii ni miongoni mwa sababu zinazochangia wananchi kutojali kile wanacho uziwa. Wapo pia wafanyibiashara walaghai huchanganya mchele wa viwango bora na ule mbaya ili kumpumbaza wanunuzi.

Huku tukivutiwa na bei ya chini ya bidhaa hiyo, tunanyima mkulima wa humu nchini haki yake na kuwapa walaghai msukumo wa kuendelea kuagiza vyakula visivyofaa kwa lengo la kujinufaisha.

Afisa katika Halmashauri ya Unyunyiziaji Maji Mashamba Nchini (NIB) Bw Daniel Nzonzo, anatamaushwa na viwango vya mchele unaoingizwa nchini na kuandaliwa na familia nyingi. Kulingana na afisa huyu, Kenya haizalishi kiwango cha kutosha cha mchele kila mwaka.

Kutokana na hayo, takribani tani 300,000 zinaagizwa nchini kila mwaka. Upungufu huu wa mchele ndio huacha mianya ya kuagiza bidhaa hiyo muhimu kutoka nje.

Na kinyume na sukari ambapo Waziri wa Kilimo amepiga marufuku uagizaji wa sukari kutoka nje, wafanyabiashara walaghai hawana vizingiti kuwazuia kuagiza mchele kutoka nje.

Katika kipindi kilichopita, Kenya imekuwa ikiagiza sukari kutoka nje ili kutosheleza mahitaji ya raia. Pia kumekuwa na malalamishi kuhusu ubora wa sukari ambayo huuzwa kwa bei ya chini na kutoka nje ikilinganishwa na sukari inayotengenezwa na kampuni za humu nchini.

Miaka miwili iliyopita, kulikuwa na ripoti za kutisha kwamba sukari iliyoletwa nchini ilikuwa na kemikali hatari kwa usalama wa afya.

Licha ya ripoti hizi, Wakenya bado wanaendelea kununua sukari kutoka nje kwa sababu ya bei nafuu na hawajali matokeo ya baadaye ya bidhaa hizi kwa maisha ya wakulima ambao huathiriwa na bei duni. Mkulima wa miwa tangu jadi ni maskini ambaye hajawahi kufurahia jasho lake kama wa nchi zingine.

Huu ndio wakati mwafaka wa kuweka mikakati ambayo itamwezesha mkulima kufurahia jasho lake.

Bw Awino hupenda kuandika kuhusu masuala ya kilimo

You can share this post!

NGILA: Tahadhari, msimu wa habari feki na kuumbuana ndio...

NGILA: Facebook ikague habari zake zisipotoshe mabilioni