• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
WANDERI: Mikopo hii ya kigeni imegeuka utumwa

WANDERI: Mikopo hii ya kigeni imegeuka utumwa

NA WANDERI KAMAU

KWA karne mbili zilizopita, utumwa umeibukia kuwa mojawapo ya masuala makuu ambayo yameshamiri mijadala kwenye majukwaa mbalimbali ya usomi duniani.

Baadhi ya wanaharakati na wasomi wamekuwa wakishinikiza mataifa ya Ulaya “kuwalipa ridhaa” Waafrika kutokana na biashara ya utumwa iliyofanyika barani humu mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20.

Shinikizo hizo zimetokana na imani ya nchi nyingi za Afika kwamba, biashara hiyo ndicho chanzo cha baadhi ya misukosuko ya kiuchumi na kisiasa ambayo inazikumba hadi sasa.

Imani hiyo pia inakitwa kwenye suala la ukoloni, ambalo kama utumwa, Waafrika wengi wanaamini ujio wa Wazungu kuzitawala nchi zao uliongeza masaibu yanayowakumba hadi sasa.

Bila shaka, masuala hayo mawili yameibua mdahalo na maswali kadhaa: Je, Waafrika wamechangia kwa vyovyote vile masaibu yanayowakumba? Tunapaswa kuendelea kuwalaumu Wazungu? Tumechukua hatua zipi kujikomboa dhidi ya changamoto zinazotuandama?

Ukweli ni kwamba Waafrika wanapaswa kujilaumu wenyewe. Mfano halisi ni mtindo wa Kenya kuendelea kutegemea misaada na mikopo ya mataifa ya nje.

Kufikia sasa, Kenya ina deni la kigeni la zaidi ya Sh6 trilioni. Cha kushangaza ni kuwa, baadhi ya wataalamu wa masuala ya kiuchumi wametabiri huenda deni hilo likaendelea kuongezeka ikiwa serikali haitapunguza ukopaji wake.

Mapema wiki hii, Rais Uhuru Kenyatta alielekea Ufaransa ambapo iliripotiwa anatafuta mkopo wa karibu Sh180 bilioni, za kufadhili ujenzi wa barabara ya Rironi-Nakuru-Mau Summit ya kilomita 190.

Ikulu haikutaka kuweka jambo hilo wazi kwani kumekuwa na malalamishi miongoni mwa Wakenya na wadau kuhusu tabia hii ya ukopaji.

Bila shaka, mwelekeo huu unaonyesha kuwa Kenya, sawa na nchi zingine zenye chumi za kadri, inapaswa kujilaumu kwa baadhi ya masaibu yanayoikumba.

Imani ya waanzilishi wa mataifa hayo kama vile Mzee Jomo Kenyatta (Kenya), Mwalimu Julius Nyerere (Tanzania), Kwameh Nkrumah (Ghana) kati ya wengine ilikuwa kuona nchi zao zimepata uhuru kamili kutoka kwa wakoloni.

Mashujaa hao walijituma vilivyo wakati wa harakati za ukombozi kuhakikisha kamwe nchi zao hazingerudi katika utumwa na udhalimu wa wakoloni.

Waliamini kwamba, kwa kupata uhuru nchi zao zingepata nafasi kubuni sera huru ambazo zingezifanya kujitegemea kiuchumi na kisiasa.

Hata hivyo, mkasa mkuu umekuwa ni watawala wa mataifa hayo. Kwa mfano, imebainika kuwa mataifa mengi yaliyostawi kiuchumi yamekuwa yakitumia ufadhili wa miradi mikubwa ya miundomsingi kama chambo, kuzifanya nchi zenye chumi dhalili kama Kenya kulazimika kuchukua mikopo kutoka kwake.

Hilo huhakikisha kwamba nchi hizo zinaendeleza ushawishi wake kuhusu maamuzi ya kiuchumi na kisiasa yanayochukuliwa na nchi za Afrika.

Kwenye safari yake Ufaransa, wito wetu kwa Rais Kenyatta ni kutoendelea kuifanya Kenya “mtumwa wa kifedha” kwa kuchukua mikopo ambayo imegeuka kuwa mzigo mzito kwa mlipaushuru. Akikaidi hilo, basi itakuwa sawa na kuendeleza “utumwa” wa kisasa.

[email protected]

You can share this post!

NGILA: Facebook ikague habari zake zisipotoshe mabilioni

MUTUA: Itakuwa kibarua kudhibiti Trump na Biden mijadalani