Visa vya corona vyakaribia 40,000
Na CHARLES WASONGA
KENYA Jumamosi ilikaribia kuandikisha visa 40,000 vya maambukizi ya Covid-19 watu 261 zaidi walipothibitishwa kuwa na virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa huo hatari.
Visa hivyo vipya vilifikisha idadi jumla ya maambukizi kuwa 39,184 baada ya sampuli 3,387 kupimwa ndani ya saa 24 zilizopita.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema kuwa miongoni mwa wagonjwa hao 261 wapya, 249 ni Wakenya ilhali 12 ni raia wa kigeni.
Mwenye umri mdogo zaidi ni mtoto mwenye umri wa miezi minne huku mzee zaidi akiwa na umri wa miaka 80.
Bw Kagwe alisema jumla ya wagonjwa 312 zaidi waliruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kupona hivyo kufikisha idadi jumla ya waliopona hadi Jumamosi kuwa 26, 426.
Miongoni mwao, 229 walikuwa wakihudumiwa chini ya mpango wa uuguzi nyumbani ilhali 83 walikuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali humu nchini.
Bw Kagwe alitangaza kuwa wagonjwa watatu zaidi walifariki kutokana na Covid-19 na hivyo kufikisha 728 idadi jumla ya maafa.
Kwa mara nyingine Nairobi inaongoza kwa visa vipya vya maambukizi kwa kuandikisha visa 123 vilivyothibitishwa ndani ya saa 24 ikifuatwa na Kisumu yenye visa 37.
Kaunti ya Mombasa iliandikisha visa 13, Trans Nzoia (13), Kisii (12), Kilifi (11), Uasin Gishu (8), Machakos (7), Nakuru (5), Kajiado (5), Kaimbu (5), Meru (5), Kitui (4), West Pokot (3), Nyamira (3), Garissa (2) huku Tharaka Nithi pia ikiandikisha visa viwili.