• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
Spurs wadhalilisha Man-United kwa kichapo cha 6-1 katika EPL ugani Old Trafford

Spurs wadhalilisha Man-United kwa kichapo cha 6-1 katika EPL ugani Old Trafford

Na MASHIRIKA

JOSE Mourinho alirejea uwanjani Old Trafford na kuwaongoza Tottenham Hotspur kuwapepeta Manchester United 6-1 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Oktoba 4, 2020.

Son Heung-Min na Harry Kane walifunga mabao mawili kila mmoja huku Tanguy Ndombele na Serge Aurier wakicheka pia na nyavu za wenyeji wao.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Man-United kupokezwa kichapo kinono katika mechi ya EPL nyumbani tangu wapokezwe kichapo kingine cha 6-1 kutoka kwa Manchester City mnamo Oktoba 2011.

Kichapo hicho kilikuwa kinono zaidi kwa Man-United kuwahi kupata tangu kocha Ole Gunnar Solskjaer apokezwe mikoba ya ukufunzi mnamo Disemba 2018 na kikubwa zaidi kwa kikosi hicho tangu Ed Woodward aaminiwe kuwa Naibu Mwenyekiti Mkuu mnamo 2013.

Matokeo hayo yalisaza Man-United katika nafasi ya 16 jedwalini mbele ya West Bromwich Albion, Burnley, Sheffield United na Fulham wanaokokota nanga mkiani.

Ni West Brom pekee ndio wamefungwa idadi kubwa zaidi ya mabao (13) kuliko Man-United, Fulham na Liverpool ambao kwa sasa wamefungwa magoli 11 kila mmoja.

Hata kabla ya Anthony Martial kuonyeshwa kadi nyekundu na Man-United kusalia uwanjani na wachezaji 10 pekee, Tottenham walikuwa wakitamalaki mchezo na kuonekana kuwazidi wenyeji wao maarifa katika kila idara.

Martial alionyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 28 kwa kumzaba Erik Lamela kofi wakati wakiwania mpira wa kona.

Ushindi kwa Tottenham uliwapaisha hadi nafasi ya sita jedwalini kwa alama saba sawa na Chelsea, Leeds United na Newcastle United. Mchuano huo ulikuwa wa nne katika mashindano matatu tofauti kwa Tottenham kusakata chini ya kipindi cha siku 11.

Ndio ushindi mkubwa zaidi kwa Tottenham kuwahi kusajili ugani Old Trafford tangu waipepete Man-United 6-1 mnamo Septemba 1932.

Man-United kwa sasa wanatazamiwa kukamilisha uhamisho wa fowadi Edinson Cavani na beki Alex Telles ambao huenda wakawa sehemu ya kikosi watakachokitegemea dhidi ya Newcastle United katika mchuano wao ujao ugani St James’ Park mnamo Oktoba 17.

Kwa upande wao, West Ham watakuwa wenyeji wa West Ham United mnamo Oktoba 18, 2020.

You can share this post!

MKU, Posta zaingia katika maelewano ya ushirikiano

SIHA NA LISHE: Vyakula unavyotakiwa kula kwa tahadhari au...