• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Ruto ana hasira za mkizi, hafai kuingia Ikulu – Junet Mohamed

Ruto ana hasira za mkizi, hafai kuingia Ikulu – Junet Mohamed

NA FAUSTINE NGILA

KIRANJA wa Walio Wachache katika Bunge la Kitaifa Bw Junet Mohamed amekemea ghasia zilizoshuhudiwa mjini Keno, Kaunti ya Murang’a Jumapili, akidai Naibu Rais William Ruto na wanadani wake waliandaa na kufadhili machafuko hayo.

Akihutubia wanahabari Jumatatu, mbunge huyo wa Suna Mashariki alisema Dkt Ruto “amejawa na hasira sana na hana hulka ya kuwa rais wa Kenya.”

Kulingana naye, Naibu Rais anafaa kulaumiwa kwa vurumai za Kenol ambazo zilisababisha vifo vya watu wawili na wengine wengi kujeruhiwa.

Pia, Be Mohamed alidai kuwa Dkt Ruto amepanga kuzua ghasia katika ziara yake ya mjini Kisumu ya hizi karibuni.

“Ruto anahatarisha maisha ya wananchi kwa kuendeleza siasa zake za ‘kihasla’ ambazo zimepasua nchi hii kuwa vipande viwili vya mabwanyenye na walalahoi. Kwa sasa anapanga fujo tena Kisumu. Amemtuma Eliud Owalo kukutana na vijana wikendi nzima ili kuzua vurugu atakapotua mjini humo,” alisema.

Alisema kuwa Naibu Rais anatumia uwezo wake mkubwa wa kifedha kuchochea ghasia.

“Anafaa kuzimwa. Ghasia za Kenol zilitokana na jina la Ruto. Ana hasira nyingi na anajihisi kuwa ni yeye tu anafaa kuwa rais,” akasema.

You can share this post!

EAC sasa yaungana kumuunga mkono Amina Mohamed kuwa kinara...

Kwa nini tiba mbadala ni tishio kwa wagonjwa wa saratani