Juhudi za Manchester United kusajili Dembele na Sancho zagonga ukuta
Na MASHIRIKA
JADON Sancho ambaye ni windo kubwa la Manchester United atasalia kambini mwa Borussia Dortmund huku uhamisho wa Ousmane Dembele pia kutoka Barcelona hadi Manchester United ukigonga ukuta.
Man-United wamekuwa wakihemea huduma za Sancho, 20, tangu mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20.
Kwa mujibu wa Dortmund, usimamizi hauwezi sasa kumtia Sancho mnadani hata kama wanunuzi wataweka mezani Sh14 bilioni wanazozihitaji kwa kuwa hawana muda wa kutosha kutafuta kizibo chake.
Chini ya kocha Lucien Favre, Dortmund waliweka Agosti 10, 2020 kuwa siku ya mwisho kwa yeyote ambaye alitaka huduma za Sancho kumsajili.
Kwa upande wao, Barcelona hawapo radhi kumtoa Dembele kwa mkopo na Sh14 bilioni ambazo miamba hao wa Uhispania wanadai kwa minajili ya kumwachilia Mfaransa huyo zimeonekana kuvunja motisha ya Man-United.
Dembele, 23, aliwagharimu Barcelona Sh18 bilioni alipoagana na Borussia Dortmund miaka mitatu iliyopita.
Ingawa hivyo, wingi wa visa vya marejaha na kushuka kwa ubora wa fomu, ni miongoni mwa mambo ambayo yanasukuma Barcelona kutaka kuagana na sogora huyo ugani Nou Camp.