UA WAJENGWA: Wanaouzia kandokando ya reli Githurai waruhusiwa japo kwa masharti
Na SAMMY WAWERU
MWEZI mmoja baada ya wafanyabiashara wanaouzia bidhaa kandokando ya reli eneo la Githurai kufurushwa, wameruhusiwa kuendeleza biashara zao huku ujenzi wa ua ukiendelea.
Shirika la Reli Nchini linaendelea na mikakati ya kuweka ua mita chache kutoka kwa reli, ili kuzuia watu kujenga vibanda au maduka karibu na njia hiyo ya garimoshi.
Kulingana na baadhi ya wachuuzi tuliozungumza nao, wameruhusiwa kuendeleza baishara zao kwa muda usiojulikana, utengenezaji wa fensi ukitekelezwa.
“Ilani imetolewa tusijenge vibanda wala maduka,” akasema James Gikundi, mfanyabiashara. Waliorejea kuendeleza biashara wanatandaza magunia au vyandarua ardhini, na kuruhusiwa kuweka mwavuli kujizuia dhidi ya miale kali ya jua au mvua.
Ujenzi wa ua ulianza Septemba 2020, na kufikia sasa vikingi vya saruji vimesimamishwa.
Soko hilo la reli lina zaidi ya wachuuzi 1,000 wengi wakiwa wauzaji wa bidhaa za kula na mazao ya kutoka shambani. Lilibomolewa Septemba na Shirika la Reli, kwa minajili ya ufufuzi wa usafiri na uchukuzi kwa njia ya reli kati ya jiji la Nairobi na Nanyuki.
Tayari garimoshi la abiria limeanza kuhudumu kati ya Thika na Nanyuki. Maeneo ya Githurai, Ruiru na Thika yana kituo cha reli.
Baadhi ya wafanyabiashara walioathirika wakati wa ubomoaji wa soko hilo, wametafuta sehemu mbadala kuendesha biashara zao.
“Nililazimika kukodi kibanda katika soko la Jubilee. Nina familia inayonitegemea,” akasema mchuuzi mmoja, akihimiza wenzake walioathirika kujipanga.