Kimataifa

Trump atoa maski punde baada ya kuondoka hospitalini

October 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA AFP

RAIS wa Amerika Donald Trump aliondoka hospitalini Jumatatu baada ya siku nne za matibabu ya dharura ya corona, huku akiondoa barakoa mara tu alipofika katika Ikulu ya White House, akisema ataendelea na kampeni za urais mara moja.

Kwenye ujumbe aliochapisha kwenye akaunti yake ya Twitter, Rais Trump aliwataka Waamerika wakome kuogopa virusi vya corona licha ya watu 210,000 kuangamizwa na virusi hivyo.

“Najihisi mwenye afya nzuri. Usiogope corona. Usikubali itawale maisha yako. Tumetengeneza dawa za maana. Najihisi vyema kuliko miaka 20 iliyopita!” alisema.

Katika video alizochapisha Twitter, Bw Trump alitembea peke yake kutoka hospitali ya majeshi ya Walter Reed, jijini Washington.

Kwa mbashara kwenye runinga, aliingia kwenye gari lake la kifahari huku akionyesha vidole vya gumbe hewani, kabla ya kupanda ndege ya Marine One hadi Ikulu.

Baada ya kutua White House, Trump alipanda kwenye veranda ya jumba hilo na kuiondoa maski huku akipiga saluti ya sekunde 23 kwa ndege iliyomleta ikiondoka.

“Tutaendlea na kampeni hivi karibuni,” alichapisha kwenye Twitter, ujumbe uliomkera mpinzani wake Joe Biden aliyejibu, “Waambie watu wa familia 205,000 ambao walipoteza wapendwa wao.”

TAFSIRI NA FAUSTINE NGILA