• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
TAHARIRI: Serikali isipuuze wito wa walimu

TAHARIRI: Serikali isipuuze wito wa walimu

Na MHARIRI

JUMATATU ulimwengu uliadhimisha siku ya Mwalimu Duniani yenye kaulimbiu: “Walimu: Kuongoza katika janga, kuwaza upya siku za baadaye”.

Kutokana na umuhimu wa siku hii, mashirika matatu makuu UNICEF, UNESCO na lile la ILO yalitoa taarifa ya kuonyesha kuwa walimu wana nafasi kubwa ya kufufua matumaini yetu kama ulimwengu.

Siku hii hutumiwa kusherehekea taaluma ambayo bila kuwepo, ulimwengu hauwezi kwenda mbele. Mojawapo ya malengo makuu ya baada ya Milenia ni kuhakikisha kwamba hakuna anayeachwa nyuma. Hili hutimia kupitia elimu na Mwalimu.

Janga la Covid-19 limeathiri sekta ya elimu kote duniani, ambapo wanafuzi wamekuwa nje ya shule kwa zaidi ya nusu mwaka.

Hapa Kenya, juhudi za kufungua shule hazijafanikiwa kutokana na kutotimizwa kwa baadhi ya masharti, ambayo ni muhimu kwa usalama wa wadau wote – hasa walimu na wanafunzi – dhidi ya maambukizi.

Ingawa sherehe hizo zilifanyika mitandaoni, wakuu wa vyama vya walimu – KNUT na Kuppet walikusanyika jijini Nairobi kutathmini hali ilivyo na mustakbali wa elimu baada ya janga hili.

Wziara ya Elimu ina makatibu watatu na mawaziri wasaidizi wawili. Inashangaza kwamba wizara hiyo iliona umuhimu wa kuwatuma maafisa hao kwenda kukagua jinsi taasisi za masomo ya juu zilivyojitayarisha kufungua, bila kujali kuwa ufunguzi huo utahusisha walimu.

Jumatatu wawakilishi wa walimu walitoa baadhi ya maombi ambayo kimsingi yafaa kuzingatiwa na serikali.

Kwa mfano wanataka serikali iweke mikapo kuhakikisha kuwa walimu hawataambukizwa virusi vya corona shule zitakapofunguliwa.

Kwamba walimu kuwa watapata matibabu ya bure au gya harama nafuu iwapo wataambukizwa wakiwa shuleni. Washirikishwe katika maandalizi ya kalenda ya elimu na mwongozo kuhusu jinsi ya kufidia muda ambao watoto walipoteza.

Pia serikali iongeze madarasa ili kupunguza msongamano wa wanafunzi.

Haya ni mambo yanayokwenda sambamba na mada kuu ya maadhimisho ya jana. Serikali itambue kuwa kuambukizwa Mwalimu mmoja kunaweza kuhatarisha maisha ya maelfu ya watu.

Mtoto mmoja hukutana na watu wengi kutoka shuleni hadi kwao nyumbani. Japo serikali imekuwa haiwasikizi, safari hii hoja zao si za kupuuzwa. Hili ni suala la maisha ya wengi, si la ubabe.

You can share this post!

Kiungo Michael Cuisance atua Marseille baada ya uhamisho...

Walcott arejea Southampton kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka...