Makala

BURUDANI: Alfa Ryus alianza kwa kuiga, sasa ni mwanamuziki shupavu

October 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

ALIANZIA tasnia ya muziki akiigiza vibao vilivyoimbwa na magwiji ambao wameimba nyimbo zilizoitikiwa na kuwa maarufu.

Mohamed Ali almaarufu Alfa Ryus alionelea aanze kuimba kwa kuigiza wimbo ulioimbwa na mwimbaji maarufu wa kimataifa, Diamond Platnumz wa ‘Nitampata Wapi’, akiuzindua wimbo huo akiwa kidato cha pili mnamo mwaka 2015.

Alfa Ryus hakuwa na haraka kutaka kuonyesha ubora wake kwani alionelea kwanza ajifunze kwa kuimba nyimbo zilizoimbwa na waimbaji maarufu wa Tanzania ambao walikuwa wakiwika wakati huo.

“Niliamua kufanya cover ya nyimbo ya Harmonize ya ‘Bado’ mnamo mwaka 2016 na kwa nyimbo hizo mbili za waimbaji watambulika, wapenda muziki wa Mombasa na jimbo la Pwani walitambua kwa haraka kuwa nimejitosa kwenye fani ya muziki,” alisema Ryus.

Katika pilkapilka za kuuza CD za nyimbo zake hizo mbili za cover, Ryus alikutana na mwimbaji Sinno Boy na kukubaliana kuanzisha kikundi cha Mombi Squad kwa nia nzuri ya kutaka kuinua vipaji vya uimbaji wao.

Ilikuwa mnamo Oktoba mwaka 2019, ndipo kikundi hicho cha Mombi Squad kilitoa kibao chao cha kwanza cha ‘Cheza’ ambapo tulifanikiwa kukizindua kutokana na msaada wa Harmontage wa Sika Production.

Hata hivyo, umoja wa waimbaji hao wawili haukudumu kwani kulitokea kutokubaliana kwa mambo kadhaa na hivyo wakaepukana mnamo Februari, mwaka huu na Ryus akiapa kuendeleza kipaji chake kwa nia ya kuwa mmoja wa waimbaji watajika wa Mombasa.

Mohamed Ali almaarufu Alfa Ryus. Picha/ Abdulrahman Sheriff

“Sina budi kumshukuru Harmontage kwa msaada anaonipa ambao nina hakika nitapiga hatua kubwa ya kuendeleza kipaji cha uimbaji wangu,” akasema Ryus huku akimsifu mkurugenzi huyo wa Sika Production kwa anavyosaidia chipukizi wanaoinukia kimuziki.

Mwanamuziki huyo aliandalia mashabiki wake wimbo wake binafsi wa ‘Itetemeshe’ ambao aliuzindua Aprili 2020; wimbo ambao umempa jina kubwa na wapenda muziki zaidi ya 1,500 kuusikiliza kupitia kwa YouTube.

Wimbo wake wa pili wa ‘Godown’ aliutoa mnamo mwezi wa Juni ikiwa ni ya mtindo wa Dancehall uliopendwa zaidi na mashabiki wanaopenda kucheza densi. Mnamo Agosti 11, 2020, Ryus alitoa kibao kingine cha ‘Nimechoka’ ambacho kinaendelea kuitikiwa kwa kasi.

“Ninaamini kwa msada anaonipa Harmontage na bidii nilonayo, nyimbo zangu tatu hizo na hasa hiyo ya ‘Nimechoka’ ambayo nimetoa pia video yake, nitaweza kufika mbali kimuziki,” akasema.

Kwa wakati huu, Harmontage anampangia Ryus mipango ya kufanya kolabo na waimbaji maarufu wa jimbo la Pwani wakiwemo kina Susumila, Kelechi na Shephard mbali na chipukizi wenzake kina Tingaree, Jay Wawili, Shisho D na Ma Genious.

Msanii huyo anasema anatayarisha nyimbo kadhaa ambazo hakutaka kuzitaja hadi pale atakapoamua kuzizindua kwani anaamini ni vizuri kwa wapenda muziki kujua nyimbpo mpya pale inapotolewa na si kabla.

Kati ya mipango aliyo nayo Ryus ni pamoja na kufanya ziara ya kutembelea jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania kwa ajili ya kumuona mwimbaji anayemfuatilia zaidi, Diamond kwa ajili ya kupata mawaidha na pia kujaribu kusaidika kutoa kibao kimoja na Wasafi.

“Nina haja kubwa ya kwenda Dar kwani nikipata fursa ya kumuona Diamond, nina hakika nitapata moja mawili ya kuinua kipaji cha uimbaji wangu. Pia nitajaribu kutafuta mwimbaji mmoja wa kike uwezekano wa kuimba naye nyimbo moja,” akasema.

Kwa wanamuziki wenzake wanaoinukia, Ryus anawaambia kuwa wawe na subra ya hali ya juu kwani hakuna mafanikio yanayoweza kupatikana bila ya kupitia changamoto kadhaa.