Habari Mseto

Vijana washauriwa wajiepushe na vitendo vya kuleta migawanyiko

October 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kuhamasisha vijana kuhusu majukumu yao ili siku za usoni wachukue usukani wa uongozi.

Mchungaji wa kanisa moja mjini Thika, Bw James Kariuki, aliwashauri vijana wasikubali kutumiwa vibaya na wanasiasa kwa manufaa yao wenyewe.

“Ninatoa wito kwa vijana popote walipo wasikubali kutumiwa vibaya na viongozi wachache wanaojitakia makuu. Vijana wanastahili kuhamasishwa kwa kuonyeshwa jambo la kufanya maishani,” akasema Bw Kariuki.

Alisema katika siku za hivi karibuni vijana wengi wameingizwa katika mawazo ya ukabila jambo ambao ni hatari kwa kazazi kijacho.

Alisema vijana wengi wasio na ajira wakipewa mwongozo unaostahili bila shaka watakuwa na mwelekeo na jambo la kujivunia.

Mchungaji huyo aliyasema hayo mnamo Jumatatu mjini Thika alipotoa ushauri kwa zaidi ya vijana 100 walipofika kwa hamasisho kuhusu wanachostahili kufanya maishani.

Alisema serikali ina njia nyingi za kuwafikia vijana na kwa hivyo ni vyema wakiondolewa kwa ufukara na kupewa jambo la kufanya watakuwa watu wa kutegemewa.

“Ninaipongeza serikali kwa kuwaajiri zaidi ya vijana 200,000 katika mradi wa ‘Kazi Mtaani’. Hatua hiyo imeleta mwelekeo mwema katika jamii zote nchini ambapo hata familia nyingi sasa zinapata chakula,” alisema Bw Kariuki.

Alipendekeza kwa serikali kuwapa mikopo ya fedha vijana hao ili waanzishe miradi tofauti ya kujiendeleza.

Kuhusu ulipaji wa ushuru, alisema maafisa wa idara hiyo wanastahili kuzuru mashinani ili kuwahamasisha wanaoishi huko jinsi ya kuwasilisha rekodi za mapato ya ushuru ya kila mwaka yaani KRA Returns.

Alisema ni watu wengi ambao hawana ufahamu maalum jinsi mapato hayo huwasilishwa ifikapo mwishoni mwa mwaka.

Alisema watu wengi huletewa arifa wakiagizwa walipie mapato ya ushuru kutokana na biashara zao lakini wamekuwa hawaelewi chochote kuhusu mpango huo.