Michezo

Afueni tele AFC Leopards wakipata udhamini wa Galana Oil Kenya

October 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA mara 13 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), AFC Leopards, wamepigwa jeki kifedha baada ya kampuni ya Galana Oil kufadhili mechi zao za kujifua kwa kampeni za msimu ujao wa 2020-21.

Leopards walikabiliwa na panda-shuke tele za kifedha msimu uliopita wa 2019-20 na ufadhili wa sasa ambao wamepokea ni afueni kubwa kwa wanasoka na benchi nzima ya kiufundi.

“Leopards wameingia ubia na Galana Oil Kenya, kampuni ambayo sasa itadhamini maandalizi yetu kwa minajili ya msimu ujao,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na usimamizi wa Leopards.

Galana Oil Kenya Limited ndiyo inayoendesha vituo vya mafuta vya Delta Service katika maeneo mbalimbali ya humu nchini na huuza pia oili aina ya ENOC Lubricants nchini Kenya.

Leopards ambao wamekuwa wakiandalia kwa msimu ujao, wanatarajiwa sasa kupiga kambi mjini Eldoret kwa kipindi cha siku 10 kabla ya kukamilisha maandalizi yao uwanjani Bukhungu, Kakamega na kurejea Nairobi kufikia Novemba ambapo msimu mpya wa Ligi Kuu ya humu nchini unatarajiwa kuanza.

Mnamo Juni 2020, Leopards walifaulu kuingia ubia na kampuni ya mchezo wa kamari ya BetSafe itakayokuwa ikiwapa miamba hao wa soka ya Kenya kima cha Sh40 milioni kila mwaka.

“Tuna furaha kutangaza ushirikiano huu na Galana Oil. Ufadhili huu una umuhimu mkubwa kwa kikosi ambacho kwa sasa kitajiandaa kwa utulivu na namna inavyostahili,” akasema Mwenyekiti wa Leopards, Dan Shikanda.

Hatua ya AFC Leopards kuchelewesha mishahara ya wanasoka mara kwa mara iliwashuhudia wakiagana na wachezaji Vincent Habamahoro, Ismail Diarra, nahodha Soter Kayumba, Tresor Ndikumana na kocha raia wa Rwanda, Andre Casa Mbungo.

Whyvonne Isuza, Brian Marita, John Makwatta pia walibanduka na kuyoyomea kambini mwa Wazito FC, Tusker FC na Zesco United (Zambia) mtawalia.

Leopards wanalenga sasa kujinyanyua katika soka ya humu nchini baada ya kushuhudia ukame wa miaka 22 bila taji lolote la Ligi kuu ya Kenya (KPL).

Leopards ambao hawajafichua mchezaji yeyote waliyemsajili muhula huu, wanatazamiwa kutoa taarifa rasmi kuhusu mikakati yao ya usajili katika soko la uhamisho wiki ijayo.