KINA CHA FIKIRA: Ukiogopa kuvumilia kubeba mzigo wa mateso utateseka zaidi
Na WALLAH BIN WALLAH
UVUMILIVU huleta mafanikio katika maisha.
Mtu anayevumilia kufanya kazi kwa bidii huyavuna matunda ya uvumilivu wake.
Lakini mtu wa kukaa bure anayeogopa kufanya kazi, hujisababishia njaa, mateso na majuto maishani!
Ukiogopa kuvumilia kufanya kazi, utateseka zaidi!
Vijana watatu, Peto, Pote na Pato waliishi katika kijiji cha Walavyote. Ukame ulitokea kijijini hapo baada ya mvua kuacha kunyesha kwa muda mrefu. Mimea yote ilikauka mashambani. Chakula kiliadimika kabisa! Watu waliteseka kwa njaa! Hapo ndipo vijana hao watatu walipoamua kuondoka asubuhi kuenda kutafuta angalau matunda msituni walete wakale na jamaa zao.
Kila mmoja alibeba mkoba wake na chupa ya maji ya kunywa! Walitembea kwa muda mrefu wakafika katika msitu ulioitwa Nguvukwisha saa sita na nusu adhuhuri. Jua lilikuwa la kuchoma kama pasi! Walichoka sana kwa njaa! Msitu wote ulikuwa mkavu! Hawakuona dalili yoyote ya matunda kwenye miti iliyokauka msituni!! Walikataa taa! Wakaamua kurudi kijijini kwao Walavyote. Lakini kabla ya kuanza safari ya kurudi, waliketi chini kupumzika kidogo.
Mara walisikia sauti kutoka hewani ikisema,”Vijana rudini nyumbani! Msitu huu si salama sana! Lakini msirudi mikono mitupu hivyo! Kila mtu achukue mawe hayo mnayoyaona hapo chini abebe kadri ya uwezo wake apeleke nyumbani!” Sauti ilirudia, “Chukueni mawe myapeleke nyumbani!” Walishangaa!
Peto na Pote waliyaokota mawe machache tu wakilalamika, “Jua kali hivi na njaa, halafu mtu ajibebeshe uzito wa mawe apeleke kijijini!?” Lakini Pato alichukua mawe mengi akajaza mkoba wake pamoja na mifuko ya suruali yake ya dangrizi (jeans). Alitembea kwa shida kuelekea nyumbani lakini alivumilia uzito!
Peto aliyatupa mawe yake njiani akabaki na jiwe moja tu! Naye Pote alifika nyumbani na mawe mawili tu! Kijana Pato alifika nyumbani akiwa na mawe mengi aliyoyajaza mkobani na katika mifuko ya suruali yake!
Waliwasili kijijini Walavyote jioni jua likizama. Kila mmoja alienda nyumbani kwao. Wazazi na ndugu waliwapokea kwa hamu ya kutaka kujua walikotoka na walileta nini? Kumbe walipofika nyumbani mawe yote yaligeuka yakawa matunda mazuri matamu sana! Peto aliyefika na jiwe moja, aliwaletea watu wake tunda moja tu zuri! Naye Pote aliyebeba mawe mawili, alileta matunda mawili mazuri! Pato aliyevumilia kuyabeba mawe mengi alileta nyumbani matunda mengi mazuri matamu ambayo waliyala kwa muda wa miezi mitatu mpaka mvua iliponyesha tena chakula kikapatikana mashambani!
Ndugu wapenzi, hivyo ndivyo maisha yalivyo. Mafanikio ni siri kubwa iliyofichwa ndani ya uvumilivu na kujituma kufanya kazi kwa bidii bila uzembe wala ugoigoi. Ukivumilia utafanikiwa! Lakini ukiogopa kuvumilia kuubeba mzigo wa mateso, utateseka zaidi katika dunia! Vumilia!!