• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
AFC Leopards tayari kuanika silaha mpya walizojitwalia muhula huu

AFC Leopards tayari kuanika silaha mpya walizojitwalia muhula huu

Na CHRIS ADUNGO

BAADA ya majuma kadhaa ya kusubiri, mabingwa mara 13 wa Ligi Kuu ya Kenya, AFC Leopards sasa wanatarajiwa kutambulisha wanasoka wapya walioingia kambini mwao muhula huu kwa mashabiki wiki ijayo.

Licha ya wingi wa tetesi ambazo zimekuwa zikihusisha Leopards na wachezaji wa klabu mbalimbali za humu nchini, vinara wa kikosi hicho wamesalia kimya kuhusu kiwango cha kujishughulisha kwao katika soko la uhamisho kwa minajili ya msimu ujao wa 2020-21.

Mwenyekiti Dan Shikanda, ambaye amekataa kufichua majina ya wachezaji wapya waliowasajili hadi kufikia sasa, amesisitiza kwamba walitwalia wanasoka watano pekee walioridhisha vinara wa benchi ya kiufundi.

Mbali na fowadi Harrison Mwendwa wa Kariobangi Sharks, masogora wengine ambao waliwahi kuhusishwa na uwezekano mkubwa wa kusajiliwa na Leopards ni mshambuliaji wa zamani wa Kakamega Homeboyz, Peter Thiong’o na Fabrice Mugheni ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo).

Leopards hata hivyo, wamethibitisha kuagana rasmi na wavamizi Vincent Oburu na Christopher Oruchum walioyoyomea Wazito FC na Tusker FC mtawalia.

“Tutafichua rasmi wachezaji tuliowasajili wiki ijayo kisha kuwatambulisha kwa mashabiki na benchi ya kiufundi,” akasema Shikanda.

“Hatukutaka kusajili idadi kubwa ya wachezaji ambao watatatiza makocha kuwachezesha au watavuruga usimamizi iwapo watakosa nafasi ya kuchezea kikosi cha kwanza. Tuliendea wanasoka wachache wa haiba kubwa ambao tunaamini wataleta nguvu mpya, tajriba pevu na uzoefu utakaotutambisha vilivyo,” akasema Shikanda.

Shikanda alikataa kuzungumzia suala la iwapo Leopards watamwajiri kocha mpya au la.

Wiki moja iliyopita, ilifichuka kwamba Leopards walikuwa pua na mdomo kumpa mikoba kocha wa zamani wa Township Rollers nchini Botswana, Thomas Trucha.

Ingawa hivyo, Shikanda alishikilia kwamba mkufunzi wao wa sasa, Anthony Kimani, atasalia kudhibiti mikoba ya Leopards ambaye aliongoza Leopards kusajili matokeo ya kuridhisha katika msimu wa 2019-20.

You can share this post!

Sababu za kushuhudiwa kwa idadi kubwa zaidi ya mabao katika...

TAHARIRI: Tuunge juhudi za kuukabili ufisadi