• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:55 AM
Giroud ashikilia nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote Ufaransa

Giroud ashikilia nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote Ufaransa

Na MASHIRIKA

FOWADI wa Chelsea, Olivier Giroud sasa ndiye anashikilia nafasi ya pili kwemye orodha ya wafungaji bora wa muda wote katika timu ya taifa ya Ufaransa.

Nyota huyo alimpiku nguli Michel Platini mnamo Oktoba 7, 2020, kwa kufunga mabao mawili na kuongoza Ufaransa kusajili ushindi wa 7-1 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Ukraine.

Mechi hiyo ilikuwa ya 100 kwa Giroud kuchezeshwa na timu yake ya taifa.

Giroud, 34, sasa anajivunia jumla ya mabao 42, tisa pekee nyuma ya mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Thierry Henry.

Chipukizi Eduardo Camavinga, 17, aliwafungulia Ufaransa ukurasa wa mabao katika dakika ya tisa.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Camavinga kuwajibishwa ndani ya jezi za Ufaransa na akaweka historia ya kuwa mwanasoka wa pili mchanga zaidi kuwahi kufunga bao katika timu ya taifa.

Corentin Tolisso, Kylian Mbappe na Antoine Griezmann walifunga mabao mengine ya Ufaransa ambao chini ya kocha Didier Deschamps, walinufaika pia na goli la Vitaliy Mykolenko aliyejifunga.

Viktor Tsygankov alifunga bao la Ukraine katika dakika ya 53 na kufanya mambo kuwa 4-1 jijini Paris, Ufaransa.

Kichapo hicho ndicho kinono zaidi kwa Ukraine kuwahi kupokezwa katika historia yao.

Timu hiyo ya taifa sasa inatiwa makali na fowadi wa zamani wa AC Milan na Chelsea, Andriy Shevchenko.

You can share this post!

Westgate: Korti kuhukumu wawili

Mkutano wa Ruto Kwale wazimwa