Habari Mseto

Wabunge watekwa na densi ya 'Jerusalema'

October 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wataahirisha kikao cha Jumanne wiki ijayo kujiunga na wimbi la densi maarufu kama “Jerusalema Challenge” inayohimiza ushirikiano na moyo wa kuwajali waathiriwa wa janga la Covid-19.

Kiongozi wa wengi Amos Kimunya, Alhamisi aliwataka wabunge kujitokeza kwa wingi kwa kufanya mazoezi ya densi hiyo Jumatatu na Jumanne wiki ijayo na pia kunakiliwa kwa filamu yake – shooting –  Jumatano, Oktoba 14, 2020.

“Densi hiyo itaongozwa na Spika Justin Muturi mwenyewe na nawahimiza mjitokeze kwa wingi. Pia itakuwa nafasi murwa ya kufanya mazoezi ya viungo,” Bw Kimunya akawaambia wabunge katika kikao cha Alhamisi.

Wakuu wa idara mbalimbali katika bunge na wafanyakazi wengine pia watashiriki katika mazoezi na kurekodiwa kwa filamu kuhusu densi hiyo.

Kiongozi huyo wa wengi ambaye ni Mbunge wa Kipipiri alisema densi hiyo maarufu kama “Jerusalema Challenge” itatumiwa kuonyesha kazi za bunge na “kuonyesha kuwajali waathiriwa wa Covid-19.”

Ushirikiano

Kauli ya Bw Kimunya iliungwa mkono na Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo ambaye alisema kushiriki kwa wabunge katika densi hiyo kutawapa nafasi ya kuthibitisha kuwa changamoto mbalimbali zinaweza kukabiliwa kupitia ushirikiano wa watu wa mataifa na tabaka mbalimbali.

Mbunge huyo aliahidi kwamba wenzao katika seneti wataungana nao katika mpango huo.

“Mheshimiwa Spika tumeshukuru kwa usaidizi ambao afisi yako imetupa kushiriki mazoezi kwa ajili ya kunakili filamu ya densi ya ‘Jerusalema’,” akasema Bi Odhiambo.

Naye Mbunge Maalum David Sankok alisema amefanya mazoezi mara kadha na anasubiri kwa hamu kusakata densi pamoja na Spika Muturi pamoja na wabunge wenzake.

“Nimekuwa nikifanya mazoezi kwa kutumia mikongojo yangu. Naamini kama ungekuwa hapo ungefurahi. Nawaalika Jumatatu mje tusakate densi na nitawafundisha mitindo na miondoko mipya,” akasema mbunge huyo.

Maelfu ya watu kote ulimwenguni, wakiwemo makasisi, maafisa wa polisi, mawaziri, wahudumu wa afya, wanahabari na wengine, wameweka video mitandaoni wakisakata densi kwa midundo ya wimbo huo wa injili.

“Jerusalema” ni wimbo uliotungwa na mwimbaji kutoka Afrika Kusini, Master KG (Jina lake halisi ni; Kgaogelo Moagi) na ambao umeibua msisimko kote ulimwenguni.

Wimbo huo umeidhinishwa na marais na makasisi kama wa kutoa himizo la kuwepo kwa umoja na ushirikiano katika vita dhidi ya Covid-19 kote ulimwenguni.

Wiki jana, “Jerusalema Dance Challenge” iliidhinishwa na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa wakati ambapo nchi hiyo inapanga kufungua uchumi wake.