Michezo

Isuzu East Africa kumpokea Kipchoge kishujaa wiki ijayo

October 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KAMPUNI ya Isuzu East Africa imefichua mipango ya kumpa Eliud Kipchoge ambaye ni balozi wa mauzo wa bidhaa zake mapokezi ya hadhi kubwa atakaporejea humu nchini wiki ijayo kutoka Uholanzi.

Bingwa huyo wa dunia na mshikilizi wa rekodi ya dunia kwenye mbio za kilomita 42, aliyoyomea Uholanzi kukutana na wasimamizi wake, Global Sports Communications, baada ya kushiriki London Marathon mnamo Oktoba 4, 2020 na kuambulia nafasi ya nane.

Duncan Muhindi ambaye ni Meneja wa Mawasiliano wa Isuzu East Africa, amempongeza Kipchoge kwa ushujaa wa kuhimili hali mbaya ya hewa na kukamilisha mbio za London Marathon licha ya maumivu yaliyochangiwa na tatizo kwenye sikio lake la kulia wakati wa kivumbi hicho.

“Tunapongeza Kipchoge pamoja na Wakenya wote walioshiriki mbio za London Marathon. Kipchoge alidhihirisha uanaspoti mwema kwa kuhimili maumivu kuanzia hatua ya kilomita 25 na kukamilisha mbio hizo. Huo ni ushindi mkubwa kwa Wakenya na funzo kubwa kwa wanamichezo wetu,” akasema Muhindi.

Vincent Kipchumba aliambulia nafasi ya pili kwenye kitengo cha wanaume baada ya kuzidiwa maarifa na Mwethiopia Shura Kitata. Kwa upande wa wanawake, Brigid Kosgei alihifadhi ubingwa wa London Marathon huku Ruth Chepng’etich akiambulia nafasi ya tatu nyuma ya Sara Hall wa Amerika.

“Wakenya hawa walipeperusha vyema bendera yetu jijini London. Japo Kipchoge hakuibuka mshindi, ukakamavu wake wa kujituma na kuvumilia changamoto tele katika juhudi za kutetea ubingwa wake jijini London unastahili kuwa himizo kwa wengine,” akasema Muhindi.

“Tunatambua kwamba matarajio ya Kipchoge kuhifadhi taji la London Marathon yalikuwa ya kiwango cha juu, japo jukumu hilo halikuwa rahisi. Isuzu East Africa inamhakikishia Kipchoge uungwaji mkono na kutambua kwamba ndiye mkimbiaji wa haiba kubwa zaidi wa marathon duniani,” akaongeza.

Isuzu East Africa iliwahi kumtuza Kipchoge magari mawili aina ya Isuzu D-Max pickups kwa kuweka rekodi mpya ya dunia ya saa 2:01:39 kwenye marathon alipoibuka mshindi wa Berlin Marathon, Ujerumani mnamo 2018 na alipoweka historia ya kuwa binadamu wa kwanza kuwahi kukamilisha mbio za marathon chini ya saa mbili.

Kipchoge alisajili muda wa saa 1:59:40 aliposhiriki mbio za INEOS Challenge jijini Vienna, Austria mnamo 2019.