Sonko avuliwa nguo zaidi

COLLINS OMULO na BENSON MATHEKA

GAVANA wa Kaunti ya Nairobi, Mike Mbuvi Sonko, anaendelea kupunguziwa mamlaka yake huku Idara ya Huduma ya jiji la Nairobi (NMS) ikiimarika na kutengewa pesa zaidi.

Katika hatua ya kumfifisha zaidi Bw Sonko, bunge la kaunti ya Nairobi lilitengea NMS Sh27. 1 bilioni katika bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2020/2021 huku serikali ya kaunti ikitengewa Sh6.4 bilioni pekee katika bajeti ya jumla ya Sh35.5 bilioni.

Hii inaendeleza masaibu ya Bw Sonko ambaye amekuwa akidai NMS ilitwaa majukumu ambayo hakuhamisha kwa serikali ya kitaifa kwenye mkataba aliotia sahihi ikulu Februari 2020.

Bw Sonko anakabiliwa na kesi tatu za ufisadi, mbili ambazo alishtakiwa majuzi alipokuwa akilumbana na Mkurugenzi wa NMS, Meja Jemedari Mohamed Badi na kutishia kubatilisha mkataba wake na serikali ya kitaifa.

Mahakama ilimzuia kukanyaga ofisi yake hadi kesi hizo zitakapoamuliwa.

Baada ya kuongezewa kesi za ufisadi, Bw Sonko alinyamaza huku Bw Badi akiendelea kusifiwa kwa utenda kazi bora.

Kiasi kikubwa cha fedha alizoachiwa Bw Sonko zitatumika katika ulipaji wa mishahara. Bunge la Kaunti ya Nairobi liilisalia na Sh2 bilioni.

Ikizingatiwa umuhimu wa NMS katika kuendesha masuala ya kaunti, bunge lilikubali mapendekezo yote yaliyotolewa na Bw Badi ambaye sasa ameongezewa Sh12.4 bilioni zaidi ikilinganishwa na bajeti ya kaunti ya Nairobi mwaka uliopita

NMS itatumia Sh18.04 bilioni kuwalipa wafanyakazi wake mishahara na Sh9.1 bilioni zilizosalia zitatumika katika miradi ya maendeleo.

Kinaya ni kwamba, licha ya kupokonywa pesa, mswada huo utafikishwa kwa Gavana Sonko ili autie saini.

“Tumetenga fedha na kukubali kila ombi la NMS na pia majukumu yaliyohamishwa kutoka kwa serikali ya kaunti,” akasema Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika bunge la kaunti, Robert Mbatia akisoma mswada wa mgao wa fedha mwaka wa 2020 katika Kaunti ya Nairobi mnamo Alhamisi.

NMS inahusika na utekelezaji wa miradi katika sekta nne muhimu katika Kaunti ya Nairobi. Sekta hizo ni Afya, Uchukuzi, Miundo Mbinu na Idara ya Mipango na Maendeleo ya Kaunti.

Kwenye bajeti hiyo, Sh7.2 bilioni zilitengewa sekta ya Afya, Sh3.7 bilioni kwa masuala ya usimamizi na uongozi wa kaunti, Sh2.4 bilioni kusimamia Mazingira na Maliasili huku sekta ya ukaguzi wa miradi ikitengewa Sh1.63 bilioni.

Sekta ya uchukuzi itapokea Sh1.3 bilioni, Kawi (Sh2.3 milioni) na Mipango ya Jiji na Ardhi (Sh244.5 milioni).

Hata hivyo, kupitishwa kwa bajeti hiyo hakutakuwa rahisi huku Kiongozi wa wachache na Naibu Mwenyekiti wa kamati ya bajeti Michael Ogada akisema walilazimika kupatanisha NMS na City Hall. Pande zote mbili ziliwasilisha makadirio tofauti ya bajeti kwa kamati hiyo.

“Tulilazimika kuoanisha stakabadhi hizo mbili ili tuibuke na moja inayokubalika. Haikuwa kazi rahisi kwa kuwa kila afisi ilitaka ipokezwe fedha zote,” akasema Bw Ogada.

Kiongozi wa wengi Abdi Guyo naye alitoa wito kwa Bw Sonko na Meja Badi wakome kuvutana kwa kuwa misimamo yao mikali ndiyo ilichangia kuchelewa kupitishwa kwa makadirio ya bajeti. Hata hivyo, alisema afisi zote mbili zilipewa kiwango kinachostahili wala hakuna mrengo uliobaguliwa.

“Tulijua kwamba utata ungetokea kwenye mchakato wa kuandaa bajeti hii lakini ajenda ya Rais Uhuru Kenyatta haiwezi kuafikiwa iwapo baadhi yetu tutajaribu kusababisha migawanyiko. Tunahitaji kaunti iimarishe utoaji wa huduma,” akasema.

Hata hivyo, Diwani wa Ngara Chege Mwaura alizua hoja akishangaa jinsi bajeti hiyo itafadhiliwa ikizingatiwa kaunti hiyo haijakuwa ikitimiza malengo yake katika ukusanyaji wa fedha.

Habari zinazohusiana na hii

Maseneta roboti

Sonko azongwa

Sonko nje

Sonko ajua hajui

Ni gavana spesheli?