TAHARIRI: Ni haki ya mawakili nchini kuandamana
Na MHARIRI
HATUA ya Mahakama Kuu kukataa ombi la kuzuia Chama cha Mawakili nchini (LSK) kuandamana katika majengo ya bunge kumshinikiza Rais Uhuru Kenyatta kuvunja bunge ni ya kutia moyo.
Hii ni kutokana na ukweli kuwa haki ya raia kuandamana imekuwa ikikabiliwa na hatihati katika miaka ya hivi karibuni. Jaji Weldon Korir alisema mawakili hawawezi kuzuiwa kutekeleza haki yao ya kuandamana mradi tu wafanye hivyo kwa kuzingatia sheria.
LSK ilimpa Rais Kenyatta hadi Oktoba 12 avunje bunge kwa kushindwa kutunga sheria ya kuhakikisha usawa wa jinsia alivyoshauri Jaji Mkuu David Maraga.
Bunge la Taifa na lile la Seneti liliwasilisha ombi wakati wa kusikizwa kwa kesi iliyowasilishwa baada ya ushauri wa Jaji Maraga wa kuvunjwa kwa bunge.
LSK inapanga maandamano kuanzia Jumatatu wiki ijayo kama njia ya kumshinikiza Rais Kenyatta atekeleze ushauri wa Bw Maraga.
Kama alivyodokeza Mwenyekiti wa LSK, Nelson Havi, maandamano hayo yaruhusiwe maadamu kusiwe na visa vya uvunjaji wa sheria.
Ikumbukwe kuwa mengi ya mageuzi yaliyopatikana humu nchini yametokana na maandamano kama haya ya kushinikiza tawala zilizopita kuheshimu haki kama msingi wa kutii maagizo ya mahakama.
LSK imeshikilia kwamba Rais Kenyatta hana budi ila kukumbatia ushauri wa Jaji Mkuu wa kuvunja bunge huku pia ikiitaka Wizara ya Usalama wa Ndani iwaondoe walinzi wote wa wabunge na maseneta.
Kwa vile hili la kushinikiza rais avunje bunge si la mawakili pekee, maafisa wa Chama cha UGM, wakiongozwa na aliyekuwa Naibu Gavana wa Nairobi Jonathan Mueke na mbunge wa zamani wa Ndhiwa, Agostino Neto walijiunga na LSK kuwashawishi Wakenya waungane nao kumshinikiza Rais avunje bunge.
Hata hivyo, Jaji Mkuu Maraga bado hajabuni jopo la majaji watatu kusikiza na kuamua kesi iliyowasilishwa mahakamani kuhusiana na ushauri wake ambao umezua maoni mseto miongoni mwa wabunge na maseneta.