Makala

MWANAMUME KAMILI: Tatizo ni baadhi yetu huwa tunaenda na mawimbi tu!

October 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na DKT CHARLES OBENE

KILA mtu yuko mbioni kutafuta kile ambacho mwenyewe hana!

Si pesa, si akili, si wanawake, si wanaume, si mashangingi, si magogo ya watu.

Kila mja anatafuta angalau kitu kinachomfaa ama anachodhani kitamfaa. Tatizo ni kwamba baadhi yetu tupo humu humu tu. Tunakwenda kwa mawimbi na kasi ya dunia ila hatuna habari tuendako. Majanga ya watu hasa!

Tumevishwa gwanda la mfumo wa “soko huru” japo wengine hatuelewi kitu kuhusu soko ama uhuru uliopo sokoni.

Gumu zaidi ni kwamba binadamu hawaishi pilkapilka za kutafuta na kutafutana kwa namna moja ama nyingine. Mwisho wa siku, “kila mtu yuko sokoni akitafuta kile ambacho mwenywe hana!” Ewe msomaji, sijui unachokitafuta kama kweli unatafuta kitu. Lakini kuna mambo ya msingi katika maisha ya binadamu yasiyostahili mzaha. Kweli, sharti kila mja kujua vyema mwanzo na mwisho wa mchezo. La sivyo, tutasalia sokoni tukitafuta tusichokijua ama kufanikiwa kukipata tusichokihitaji. Kutia chudi kutafuta usichokijua ama kusherehekea kupata usichokihitaji ni wamoja! Ole nyinyi wenye hamasa mnaofukuzana na magogo ama mnaoguguna mawe kwa kuwa soko ni huru. Kila mtu anachagua kile kitu ambacho hana.

Punde tu tangazo la “vyuo kufunguliwa tena” lilipogonga ndewe za malofa, wameibuka wabishani wanaopinga uamuzi wa serikali.

Hawataki watoto kwenda shule muhula huu. Kisa na maana? Eti mbuzi wametafuna sare za wanafunzi. Eti wanafunzi walichezea wakazichanachana sare walipokuwa likizoni. Eti wanafunzi wamekula wakatononoka mili na sare zenyewe si zao tena. Eti wazazi wamekula karo na masurufu ya wanafunzi. Wenye hofu wanaona “njama ya serikali kuwamalizia watoto!” Wengine wanapinga kufunguliwa vyuo kwa hofu ya “kuambukizwa corona kutoka shuleni!” Yote kenda. Kumi, wabishani hawa “wanaomba serikali kuwapa watoto muda kujifungua kabla kwenda shuleni” Hili la “watoto kujifungua” ndilo wazo linaloashiria hekima, akili, mawazo na tafakuri za wengi wanaojifanya kuwa wazazi wa leo.

Nilidhani kwamba wanaume kwa wanawake wa leo wanaishi kwa mpangilio.

Wanazaa na kuzalishana huku wameshikilia kamba ya malezi pamoja. Wanalala na kuamkia wazo moja. Iweje sasa tunafukiza umbea na ubishani katika masomo ya wanafunzi wanaotaka jaribisha maisha yao? Iweje wanafunzi kukosa sare za shule ilhali wazazi wanabadili nguo kucha kutwa? Simama kwenye mabaa vijijini ushangae jinsi wanaume kwa wanawake wanavyotambalia magoti! Ndio wao hao wanaosuta juhudi za serikali “kuasisi masomo vyuoni!”

Dhana ya “watoto kuathirika na virusi” ni dhana ya watu waliochagua wenyewe kukalia bongo zao. Wanaohurumiwa wanacheza ovyo bila barakoa. Wamecheza wakachezea hadi sare za shule. Wamecheza nyanjani na vyumbani wakahimilika. Sasa tunawatakia muda “kujifungua kabla kwenda tena shuleni!” Lipi baya zaidi litakalowafika darasani na maktabani, tena wanakodhibitiwa kwa msingi wa sheria na adabu shuleni? Nilidhani nyie watu wazima wenye akili, lakini sivyo hali ilivyo.

Wamepewa simu na vipakatalishi wakasome lakini wapi? Wako mitandaoni wakipakua na kupakia picha na dodoki zao. Wameasi masomo wakaanza kazi ya kutafuta picha za wanawake kwa wanaume mitandaoni kisha, “Ku-Like, Ku-Share, Ku-Post! Vichwa maji hawa wanasubiri kutahiniwa mwakani ilhali hata viganja havina habari lini mwisho viligusa kalamu. Wataandika nini kwenye mabuku ya mtihani ikiwa filamu kwenye runinga ndio somo la kila siku? Isitoshe, wazazi wao na akili zao timamu hawana haya kumzomea waziri wa Elimu.

Jamani wanaume kwa wanawake wa leo kunani? Mwajipumbaza na ubishani na ulimbukeni huu badala ya kusima wima kuwaelekeza vijanajike kwa vijanadume angalau wadhihiri bongo zinazopiku hizo mlizodhihiri. Wanawake kwa wanaume ndio kwanza wanastahili kukuna kichwa vipi watainuka na kusimama pamoja kama familia.

Kuna watu walioshikamana wamekwisha jinunulia viwanja wakajenga majumba na kusitiri familia zao. Wambea na wabishani wangali kwenye mikeka wakila meno. Wangwana wamefanikisha biashara na miradi yao mbalimbali, wanasomesha watoto japo mapato ni ya kijungumeko. Wengine wanasuta serikali kwa kuwa mabinti hawana sare za shule. Sio ajabu kwamba hata watoto wenu wanasubiri kujifungua! Wa nyoka ni nyoka. Kila mtu yuko mbioni kutafuta kile ambacho mwenyewe hana!

[email protected]