Habari Mseto

Rais Kenyatta aongoza nchi katika maombi ya kitaifa

October 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY WAWERU

RAIS Uhuru Kenyatta ameongoza hafla ya maombi ya kitaifa katika Ikulu jijini Nairobi, Jumamosi.

Kiongozi wa nchi alitangaza siku tatu zitengwe mahususi kwa kufanya mfululizo wa maombi kuliombea taifa, kuanzia jana Ijumaa, Oktoba 9, 2020 hadi kesho Jumapili.

Kiongozi huyo wa nchi, alitenga siku ya leo, Jumamosi, Oktoba 10, 2020 kuwa siku spesheli kabisa ya maombi hayo.

Imehudhuriwa na viongozi wakuu serikalini, akiwemo Naibu Rais Dkt William Ruto, Mama wa Taifa na ambaye ni mke wa Rais, Bi Margaret Kenyatta, mawaziri, maspika wa mabunge yote makuu mawili, viongozi wa kisiasa, wa dini mbalimbali, miongoni mwa wengi wengineo.

Aidha, maombi hayo yameandaliwa wakati ambapo joto la kisiasa nchini limeonekana kupanda, huku serikali ikitoa amri na sheria kali kudhibiti mikutano ya hadhara inayoandaliwa na wanasiasa.

Hali hiyo imechangiwa na tofauti za kisiasa kati ya Rais Kenyatta na Naibu wake, Ruto, hasa baada ya Rais na kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuweka kando tofauti zao mnamo Machi 2018 kupitia salamu za maridhiano almaarufu Handisheki na kuahidi kuunganisha taifa.

Baadhi ya viongozi wanahimiza Dkt Ruto na Bw Raila kuzika tofauti zao kupitia salamu za maridhiano, ili kupunguza au kutuliza joto la kisiasa linaloendelea kushuhudiwa nchini.

“Joto la kisiasa nchini litapungua iwapo Naibu wa Rais, William Ruto na aliyekuwa Waziri Mku, Raila Odinga wataweka kando tofauti zao, kupitia salamu za maridhiano. Rais Uhuru Kenyatta naye awe wa tatu kuwaleta pamoja,” akasema aliyekuwa gavana wa Kiambu, William Kabogo.

Awali, Oktoba 10 kila mwaka ilikuwa ikiadhimisha Sikukuu ya Moi Dei, iliyoasisiwa na Rais Mstaafu Daniel Arap Moi ambaye kwa sasa ni marehemu.

Katiba ya sasa na iliyozinduliwa Agosti 2010 iliondoa maadhimisho hayo, nayo serikali ya Jubilee inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta ikibadilisha Sikukuu ya Kenyatta Dei, inayoadhimishwa Oktoba 20 kila mwaka kuwa Mashujaa Dei.