Makala

TAHARIRI: Vutapumzi itumike vilivyo kupunguza ajali

October 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

KWA wiki moja pekee tangu Rais Uhuru Kenyatta atangaze kufunguliwa tena kwa maeneo ya burudani, zaidi ya watu 60 wamefariki dunia kwenye ajali za barabarani.

Ajali hizi, kulingana na Mamlaka ya Usalama Barabarani (NTSA), asilimia kubwa ya waliohusika kwenye ajali hizo walikuwa walevi.

Biashara za maeneo ya burudani zinachangia uchumi wa nchi kwa kuajiri maelfu ya watu. Wawekezaji wana haki ya kuendelea kuhudumia wateja wao, hasa ikizingatiwa kuwa walikuwa wamefungwa kwa karibu nusu mwaka. Lakini uhuru huo wa kujiburudisha yafaa ufanywe kwa njia ya kukomaa na kuwajibika.

Ulevi unafahamika kuwa chanzo cha maovu mengi. Baadhi ya watu wanapolewa, hupotewa na fahamu na kusahau kanuni, sheria na maadili.

Kuna wengine ambao kwa sababu ya ulevi, hukataa kujifunga mishipi wanapokuwa kwenye magari. Baadhi huendesha magari kwa mwendo wa kasi bila ya kutii sheria za barabarani. Matokeo yake ni kuwaua watu wasiokuwa na hatia.

Katika kipindi cha miezi sita ambapo maeneo ya burudani yalikuwa yamefungwa, pamoja na safari za usiku kusimamishwa kufikia saa tatu, katika nchi nzima kuliripotiwa ajali chache mno. Hii inaonyesha kwamba tatizo la ajali hizi ni watu kuendesha magari wakiwa walevi.

Kwa hivyo mpango wa NTSA kurejesha kifaa cha kupima viwango vya ulevi mwilini mwa dereva ni mzuri. Kifaa hicho kiliacha kutumiwa 2017 baada ya mahakama kuamua kwamba kilikuwa kikitumiwa kinyume cha sheria.

Lakini sasa ni wakati bora zaidi kukitumia, ili madereva wazembe wasiojali maisha ya wengine barabarani, wakabiliwe vilivyo.

Kifaa hicho ni cha kuwezesha polisi au maafisa wanaopima madereva wajue kiwango cha ulevi na kuchukua hatua zinazofaa. Hapa ndipo ilipo changamoto. Maafisa wengi wa polisi wamekuwa wakitumia fursa za aina hii kujipatia hela za ziada. Kila kunapozuka jambo linalohimiza utekelezaji wa sheria, kuna maafisa wanaolitumia kuwa kitega uchumi.

Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai na wakuu wa NTSA wanapaswa kufuatilia kwa makini utekelezaji na utumiaji wa kifaa cha vutapumzi. Lengo lake liwe ni kulinda maisha ya wanaotumia barabara wala si kuwatafutia riziki maafisa wafisadi.