Uingereza wana kila sababu ya kutwaa taji la Euro na Kombe la Dunia – De Bruyne
Na MASHIRIKA
KIUNGO wa Manchester City na timu ya taifa ya Ubelgiji, Kevin De Bruyne anaamini kwamba Uingereza wana kila sababu ya kutawazwa mabingwa wa fainali zijazo za Euro na Kombe la Dunia.
Baada ya fainali za Euro zilizoahirishwa mwaka huu 2020 sasa kupanyiko kufanyika 2021, vikosi vya mataifa mbalimbali vitatua nchini Qatar kuwania ufalme wa Kombe la Dunia.
De Bruyne ambaye alitawazwa Kiungo Bora wa Mwaka wa Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa) na Mchezaji Bora wa Mwaka 2019-20 kambini mwa Man-City, atakuwa sehemu ya kampeni hizo.
Uingereza na Ubelgiji walitinga hatua ya nusu-fainali za Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi. Hata hivyo, Ubelgiji waliwapiga Uingereza katika mojawapo ya mechi za makundi kwenye fainali hizo kabla ya kuwapepeta Uingereza kwa mara nyingine kwenye hatua ya kutafuta mshindi nambari tatu.
Vikosi hivyo vinakutana tena leo Jumapili kwenye gozi la Uefa Nations League uwanjani Wembley, Uingereza.
“Lazima wanafurahi sana. Uingereza wana kikosi cha wanasoka wachanga walio na uwezo mkubwa uwanjani,” akasema De Bruyne, 29.
Uingereza hawajawahi kushindi taji lolote la haiba kubwa kwenye ulingo wa soka tangu walitia kapuni ufalme wa Kombe la Dunia mnamo 1966.
Kwa mujibu wa De Bruyne aliyetawazwa pia Mchezaji Bora wa Mwaka kwenye tuzo za Chama cha Wanasoka wa Kitaalamu (PFA), kubwa zaidi ambalo Uingereza wanalenga kwa sasa chini ya kocha Gareth Southgate ni kutwaa ubingwa wa mashindano yajayo ya Euro na Kombe la Dunia.
“Zipo timu nyingi zinazotamani kutia kibindoni mataji ya vipute hivyo, lakini nahisi kwamba Uingereza ndio wanaojivunia idadi kubwa ya wanasoka walio na uwezo wa kuwatambisha vilivyo na kuweka hai matumaini yao ya kutawala mashindano hayo. Na ni lazima watafanya hivyo,” akasema De Bruyne.
Maoni ya De Bruyne yameungwa na kocha Roberto Martinez wa Ubelgiji ambaye kwa mtazamo wake, mkufunzi mwenzake Southgate, ana kikosi kinachojivunia mseto mzuri zaidi wa wanasoka wazoefu na chipukizi walio na kiu ya kusajili ushindi katika takriban kila mchuano.
“Wachezaji wa Southgate wana utajiri mkubwa wa vipaji ambao una uwezo wa kutambisha timu ya taifa ya Uingereza kwenye soka ya kimataifa. Ni suala la muda tu kabla ya kikosi hicho kutwaa ufalme wa Euro, Kombe la Dunia ay mapambano hayo yote mawaili,” akasema kocha Martinez ambaye pia amewahi kunoa klabu za Swansea City, Wigan Athletic na Everton.
Uingereza kwa sasa wanashikilia nafasi ya nne kwenye orodha ya viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA). Hadi walipovaana na Ubelgiji mnamo Oktoba 11, 2020, Uingereza walikuwa wamewapepeta Wales 3-0 uwanjani Wembley. Mabao yao yalifumwa wavuni kupitia kwa Dominic Calvert-Lewin, Conor Coady na Danny Ings walioshirikiana vilivyo na kiungo Jack Grealish.
Ubelgiji ambao kwa sasa wanaongoza orodha ya FIFA, walikosa huduma za Dries Mertens na Eden Hazard katika gozi la jana la Uefa Nations League.
De Bruyne ambaye anatarajiwa kutia saini mkataba mpya wa miaka miwili kambini mwa Man-City, alijiunga na kikosi hicho mnamo Agosti 2015 baada ya kushawishiwa kuagana na VfL Wolfsburg ya Ujerumani kwa kima cha Sh7.7 bilioni.
Nyota huyo anajivunia kushindia Man-City mataji mawili ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), manne ya League Cup na Kombe la FA mara moja.