• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
Jopo la kuboresha ushirikiano kati ya mawaziri na maseneta labuniwa

Jopo la kuboresha ushirikiano kati ya mawaziri na maseneta labuniwa

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Seneti na Baraza la Mawaziri zimebuni jopo maalum litakalohakikisha kuwa maamuzi, hoja na miswada inayopitishwa na maseneta inatekelezwa na Serikali Kuu.

Jopo hilo ambalo litaongozwa kwa pamoja na Karani wa Seneti Jeremiah Nyengenye na Mkuu wa Kitengo cha Utekelezaji wa Miradi ya Rais (PDU) pia litashirikisha uhusiano kati ya maseneta na mawaziri.

Waziri wa Usalama Fred Matiang’i ndiye alitangaza kuunda kwa jopo hilo Jumatatu baada ya kuwaongoza mawaziri 10 kwenye mkutano wa mashauriano kati yao na maseneta.

Upande wa maseneta, ulishirikisha wenyeviti na manaibu wenyeviti wa kamati za bunge hilo, waliongozwa na Spika Kenneth Lusaka katika mkutano uliofanyika katika mkahawa wa Crowne Plaza, Nairobi.

“Tumekubaliana kuunda jopo au kamati maalum itakayofuatilia sheria zote zinazopitishwa katika seneti, zikiwemo hoja na maamuzi mengine yenye manufaa kwa taifa hili na wananchi kwa ujumla,” Dkt Matiang’i akawaambia wanahabari baada ya mkutano huo uliodumu kwa saa tatu.

“Wajibu mwingine wa jopo hilo utakuwa ni kupalilia uhusiano wa kiutendakazi kati ya mawaziri na maseneta. Hii itaondoa dhana inayoondelezwa na watu wengine kwamba mawaziri hawaheshimu kazi ya seneti na wamekuwa wakisususia mialiko ya kutakiwa kufika mbele ya kamati zake,” akaeleza.

Waziri Matiang’i ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Kushirikisha Utekelezaji wa Miradi na Mipango ya Serikali Kuu, pia alisema kuanzia mwezi huu kuendelea mbele mawaziri na maseneta watakuwa wakikutana kila mara.

“Mikutano hii itakuwa ya kujenga uhusiano bora kati kitengo cha Afisi Kuu na Maseneta kwa sababu sote tunahudumia wananchi wetu,” akasema.

Mawaziri waliohudhuria mkutano huo ni’ James Macharia (Uchukuzi), George Magoha (Elimu), Mutahi Kagwe (Afya), Sicily Kariuki (Maji), Eugene Wamalwa (Ugatuzi) na Farida Karoney (Ardhi), Peter Munya (Kilimo), Ukur Yatani (Fedha) na Joe Mucheru (ICT).

Ujumbe wa Seneti nao ulioongozwa na Spika Kenneth Lusaka na kiongozi wa wengi Samuel Poghisio na ukajumuisha wenyeviti na manaibu wenyeviti wa kamati mbalimbali za seneti.

Kwa upande wake Bw Lusaka alimpongeza Waziri Matiang’i kwa kukubaliana kuongoza wenzake kwa mkutano na maseneti kuhusu masuala ya kiutendakazi.

“Ushirikiano wa karibu kati ya mawaziri na maseneta uchangia pakubwa katika ufanisi wa bunge la seneti. Kazi hii ni ya faida kuwa Wakenya ambao wanawakilishwa na maseneta hawa,” akasema Bw Lusaka.

Wenyeviti wa kamati za seneti wamekuwa wakilalamika kuwa maseneti hukaidi mialiko ya kutakiwa kufika mbele ya kamati zao, hali inayoathiri utendakazi wa kamati hizo.

Baadhi ya mawaziri ambao wameelekezewa lawama hizo ni Dkt Matiang’i mwenyewe, Bw Macharia (Uchukuzi) Bi Karoney (Ardhi) na Kagwe (Afya).

You can share this post!

Watu 11 zaidi waangamizwa na corona

Muturi aziba mwanya ambao wabunge hutumia kutafuna maelfu