Habari Mseto

Mvurya aunga mkono mgombeaji wa Ruto Msambweni

October 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MOHAMED AHMED

GAVANA wa Kwale, Salim Mvurya, amejitosa katika kampeni za uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge cha Msambweni kwa kumuunga mgombeaji huru Feisal Bader.

Bw Mvurya alitangaza kuwa atamuunga mkono Bw Bader ambaye jana alipata cheti chake cha kumenyana kwenye uchaguzi huo wa Disemba 15 kutoka kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Gavana Mvurya aliwasihi wakazi wa Msambweni “wasidanganywe” na kile alichokitaja kuwa “wimbi la chama” akiashiria umaarufu wa chama cha ODM ambacho mgombeaji wake kwenye uchaguzi huo ni Omar Boga.

“Mimi ninajua wakati wa kampeni watu wanaleta mawimbi ya chama, lakini ninataka kuwaambia nyinyi msikubali hilo kwa sababu chama hakiwezi kuwahudumia na kuwaletea maendeleo yoyote,” akasema Bw Mvurya alipokuwa eneo la Gazi ambapo marehemu Suleiman Dori, aliyekuwa mbunge wa eneo hilo, alizaliwa.

Bw Dori ni mjombawe Bw Bader ambaye anataka kumrithi kwenye kiti hicho katika uchaguzi unaoendelea kuzua tumbo joto.

Akimpigia debe Bw Bader, Gavana Mvurya alieleza wakazi kutokubali kushawishiwa na chama cha ODM.

“Msiangalie wale ambao wanabebwa na chama kuwachagulia mtu ambaye baadaye mtajutia. Mimi najua kuwa hapa mna kijana wenu Fiesal ambaye ataendeleza maendeleo aliyokuwa ameanza pamoja na marehemu,” akasema Bw Mvurya.

Huku akiwapiga vijembe wapinzani wa Bw Bader, Bw Mvurya alisema mtu hafai kujificha chini ya chama ili achaguliwe.

“Nyinyi wakazi wa Msambweni ndio mnaowajua wale viongozi wanaotaka kiti hicho na basi msikubali mtu awachagulie. Msikubali mtu afanye uamuzi kwa niaba yenu,” akasema.

Bw Mvurya alimuidhinisha Bw Bader siku chache baada ya Naibu Rais William Ruto ambaye pia anamuunga mkono kutangaza kuwa wagombeaji wengine watatu wameamua kumuunga mkono Bader.

Dkt Ruto alikutana na Bw Peter Nzuki, Bashir Kilalo na Bw Bakari Sebe ambao wameamua kumuunga mkono Bw Bader na kuweka kando mipango yao ya kuwania kiti hicho.

Bw Kilalo ambaye alikuwa awanie kiti hicho kupitia tiketi ya ANC aliingia chama cha Kadu Asili na baadaye kuingia kambi ya Dkt Ruto na kumuunga mkono Bw Bader.

Bw Nzuki wa chama cha Democratic Party aliunga mkono upande wa Bw Ruto na kuwaacha Bw Khamisi Mwakaonje wa UGM na Abdulrahman Shee wa Wiper pamoja na Sharlet Mariam kumenyana na Bw Boga wa ODM.

Akizungumza jana baada ya kuwasilisha karatasi zake kwa IEBC, Bw Bader aliwaambia wapinzani wake wajiweke tayari kwa ushindani.

“Mimi na timu yangu sote tuko tayari kuanza kampeni. Ninataka kusisitizia watu wa Msambweni wadumishe amani kwa sababu uchaguzi ni kitu cha kuja na kitapita baada ya Disemba 15,” akasema.