Makala

Fistula inavyowahangaisha wanawake

October 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA WANGU KANURI

Yumkini ni furaha ya kila mwanamke mjamzito kumpakata mtoto wake ajapojifungua na pia kuwa mwenye siha njema.

Lakini si kila mwanamake na raha baada ya kupata mtoto kwa sababu ya kuugua nasuri ya njia ya uzazi (fistula). Nasuri inapompata mwanamke, mara nyingi hutengwa na wanafamilia na marafiki zake kwa sababu ya uvundo unaomtoka kwa kutoweza kuzuia haja.

Isitoshe, utafiti unabainisha kuwa nasuri hii humpata mwanamke akiwa na mimba yake ya kwanza. Kila mwaka, wanawake kati ya 50,000 na 100,000 duniani hupata nasuri katika njia yao ya uzazi kulingana na takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).

Nasuri humpata mwanamke baada ya kuwa na uwazi usio wa kawaida katikati ya sehemu za mwanamke za siri na njia ya mkojo. Aghalabu mwanamke hupata nasuri hii akiwa mjamzito.

Hata hivyo, mwanamke aliye na nasuri hii anaweza kupata tiba kupitia upasuaji, na ndiyo njia pekee ya kupokea matibabu.

Nasuri hii humpata mwanamke anayekawia kuenda hospitalini ilhali ana maumivu kutokana na ujauzito wake, na isitoshe hana uwezo wa kupata matibabu ya dharura ya upasuaji ili aweze kujifungua upesi.

Pili, mwanamke huyu anaweza kuwa anauhisi uchungu wa kujifunguakwa siku nyingi na uchungu huu haupungui kiasi cha kwamba mtoto huyo hufa.

Kifo cha kijusi hutokea kutokana na uchungu huo wa kujifungua kuchukua muda mrefu.  Maumivu ya leba kusukuma kichwa cha kijusi kwenye njia ya uzazi huku damu ikikosa kuenea mwilini mwa mama ipasavyo.

Kupunguka kwa damu mwilini husababisha tishu laini zilizoko mwilini mwa mwanamke mjamzito kunyauka na kusababisha mashimo katikati ya uke na njia ya mkojo.

Mama huyu hujiendea haja ndogo na kubwa na wakati mwingine zote mbili asipopata matibabu yanayostahili.

Nasuri inaweza kuzuiwa kwanza kwa kuchelewesha umri wa kupata mimba ya kwanza. Hii ni tahadhari haswa kwa wasichana wapevu wasipate mimba za mapema.

Hii ni kwa sababu msichana mjamzito yumo hatarini ya kuipata nasuri ikilinganishwa na mwanamke aliyekomaa.